Latest Post

Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Abel Makubi aliyesisimama akisema jambo kwenye kikao na watumishi wa afya katika Hospitali ya Wilaya ya Kwimba

Watumishi wa afya katika Hospitali ya Wilaya ya Kwimba wakiwa kwenye kikao na Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Abel Makubi (hayupo pichani)

NA Englibert Kayombo WAMJW - Mwanza

Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Abel Makubi ametoa muda wa siku 14 kwa baraza la madaktari pamoja na baraza la wauguzi kwenda Mkoa wa Mwanza kuzungumza na watumishi wa kada wanazosimamia ili kurekebisha na kuwajengea uelewa zaidi wa maadili ya taaluma zao.

Prof. Makubi ametoa agizo hilo akiwa Wilayani Kwimba alipokuwa ziara ya kikazi kukagua hali ya utoaji wa huduma na kuzungumza na watumishi wa kada ya afya. 

“Mabaraza mengi yamekuwa yanabaki huko makao makuu kuhukumu watu, wamejiondoa kabisa kwenye kazi ya kuwajenga watumishi, badala ya kupita huku na kuwaelekeza watumishi, wao wanasubiri kupokea malalamiko” amesema Prof. Makubi

Amesema ni lazima mabaraza yahakikishe watumishi hawafanyi makosa kwa kuwaweka katika maadili mema bila kufanya hivyo tutakuwa na watumishi wasio na sifa.

Prof. Makubi amesisitiza kuwa mabaraza yote 10 yanatakiwa kutelekeza majukumu yao ipasavyo na yote wajiwekee utaratibu wa kuzunguka na kuzungumza na watumishi kuanzia ngazi ya Mikoa hadi Wilayani

Mwisho.



Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Abel Makubi akisema jambo kwa timu ya uongozi wa afya ya Mkoa wa Mwanza kwenye kikao kazi cha kujadili vifo vitokanavyo na uzazi na watoto wachanga kilichofanyika Wilaya ya Misungwi.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Dkt. Thomas Rutachuzibwa akisema jambo kwa timu ya uongozi wa afya ya Mkoa wa Mwanza kwenye kikao kazi cha kujadili vifo vitokanavyo na uzazi na watoto wachanga kilichofanyika Wilaya ya Misungwi.

Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Tiba anayesimamia Hospitali za Rufaa za Mikoa Dkt. Caroline Damian (kulia) pamoja na Katibu wa Mganga Mkuu wa Serikali Bi. Maurine Kunambi (kushoto) wakiwa kwenye kikao kazi cha kujadili vifo vitokanavyo na uzazi na watoto wachanga Mkoa wa Mwanza.

Timu ya uongozi wa afya ya Mkoa wa Mwanza wakiwa kwenye kikao cha kujadili vifo vitokanavyo na uzazi na watoto wachanga.

Timu ya uongozi wa afya ya Mkoa wa Mwanza wakiwa kwenye kikao cha kujadili vifo vitokanavyo na uzazi na watoto wachanga.


VIFO VYA MAMA WAJAWAZITO HAVIVUMILIKI TENA" – MGANGA MKUU WA SERIKALI

Na Englibert Kayombo WAMJW - MWANZA.

Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Abel Makubi amesema kuwa Serikali haitovumia tena vifo vya akina mama wajawazito vinavyosababishwa na uzembe wa watumishi kazini.

Prof. Makubi ametoa kauli hiyo alipokuwa akifunga kikao kazi cha timu ya uongozi wa afya ya Mkoa wa Mwanza kilichofanyika Wilayani Misungwi kujadili vifo vitokanavyo na uzazi na watoto wachanga.

"vifo vya akina mama wajawazito havivumiliki tena kwa sasa hivi kwenye hii dunia ambapo tumeingia uchumi wa kati, ni lazima tutafute mbinu mpya na nzuri tuweze kuziendeleza na kuhakikisha kwamba ambaye amekuja kuleta maisha asifariki” amesema Prof. Makubi.

Amesema siyo vifo vya akina mama wajawazito tuu ndio vizuiwe bali hata vya watoto wachanga wanaozaliwa pia vidhibitiwe kwa wataalam wa afya kuhakikisha watoto hao wanazaliwa salama pia.

Prof. Makubi amesema Serikali imewekeza rasilimali nyingi kwenye sekta ya afya hivyo ni vyema matunda ya uwekezaji huo yakaenda kuonekana kupitia uboreshwaji wa huduma bora za afya ikiwemo kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi na watoto wachanga.

Amesema anashangazwa na vifo vingi vya akina mama wajawazito kutokea katika vituo vya kutolea huduma za afya na sio kwenye Jamii na kuwataka watumishi hao kujitafakari ni sehemu gani kuna changamoto ili zifanyiwe kazi na kudhibiti vifo hivyo.

“Nimefurahishwa kuona mmekutana hapa kutafakari, kwa hiyo mmeshaliona tatizo hamkusubiri Wizara ya Afya kuja kuwaambia mfanye nini, hilo ndio linanipa moyo mmejitambua na mmeamua kuchukua hatua wenyewe” amepongeza Prof. Makubi wa timu ya uongozi wa afya ya Mkoa wa Mwanza kwa kuanza kuchukua hatua.

Aidha,Prof. Makubi ametoa wito kwa Mikoa mingine iendeleze kile ambacho mkoa wa Mwanza imeanza kufanya kwa kufanya vikao vya tathimini na kuweka mikakati ya kudhibiti vifo vitokanavyo na uzazi na watoto wachanga. 

“Kabla ya mwezi wa kwanza haujaisha kila Mkoa uwe umeshakaa, ukishirikisha viongozi wote wa Mkoa, Wilaya na Halmashauri vituo vya afya mpaka zahanati wawe na wawakilishi ili mjadili mbinu ambazo zinaweza kupunguza vifo vya akina mama wajawazito kwa kiasi kikubwa zaidi”

 Amesisitiza Prof. Makubi akitoa agizo hilo kwa timu za uongozi wa afya kwa mikoa yote.“Tuondoke hapa tulipo kwa sababu wananchi wanatamani twende tupige hatua moja mbele ili tukaboreshe huduma zetu, kwa mikakati mliyoweka tukiitekeleza naamini tunaweza tukatoka kwenye tatizo hili” Amesisitiza Prof. Makubi.

Naye Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Dkt. Thomas Rutachuzibwa amesema kuwa wameyapokea maelekezo yote aliyoyatoa Mganga Mkuu wa Serikali na watayafanyia kazi kuhakikisha vifo vya akina mama wajawazito na watoto wachanga vinadhibitiwa mkoani humo.

“Ninakuahidi ndani ya miezi mitatu tutaanza kupata mabadiliko, tutakaa kwa muda uliobaki kuweka mpango kazi kuhakikisha tunaenda kutekeleza yale yote tuliyopanga ili kupunguza vifo vya akina mama wajawazito na watoto wachanga” amesema Dkt. Rutachuzibwa.

Dkt. Rutachuzibwa amesisitiza suala la wajibikaji kwa watumishi wa afya wakiwa kwenye maeneo yao ya kazi kwa kutambua wana wajibu upi na kuhakikisha wanatoa huduma bora kwa wananchi na kupunguza changamoto zilizopo maeneo yao ya kazi.

“Kila mmoja ajitambue, tutoe huduma kwa wananchi, kuanzia leo naomba wote tuanze upya, kila mtu awajibike kwa kipande chake” amesisitiza Mganga Mkuu wa Mkoa Dkt. Thomas Rutachuzibya.

Mwisho


Mkurugenzi wa Huduma za Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe kutoka Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Dkt. Ntuli Kapologwe akisema jambo kwenye kikao kazi cha kujadili vifo vitokanavyo na Uzazi na Watoto wachanga Mkoa wa Mwanza

Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza Bw. Emmanuel Tutuba akisema jambo wakati wa kikao kazi cha kujadili ivifo vitokanavyo na uzazi na watoto wachanga kwa mkoa huo

Mganga Mkuu Mkoa wa Mwanza Dkt. Thomas Rutachuzibwa akisema jambo wakati wa kikao kazi cha kujadili vifo vitokanavyo na uzazi na watoto wachanga katika mkoa huo

Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Tiba anayesimamia Hospitali za Rufaa za Mikoa Dkt. Caroline Damian (kushoto) pamoja na mwakilishi kutoka Ofisi ya Mganga Mkuu wa Serikali Bi. Maurine Kunambi (kulia) wakiwa kwenye kikao kazi cha kujadili vifo vitokanavyo na uzazi na watoto wachanga Mkoa wa Mwanza.

Mkurugenzi Mtendaji Taasisi ya Benjamin Mkapa (kulia) Dr. Ellen Mkondya- Senkoro pamoja na viongozi wengine wakiwa kwenye kikao kazi cha kujadilii vifo vitokanavyo na uzazi na watoto wachanga Mkoa wa Mwanza.

Wajumbe wa timu ya afya ya Mkowa wa Mwanza wakiwa kwenye kikao cha kujadili vifo vitokanavyo na uzazi na watoto wachanga katika Mkoa wa Mwanza.

Na Englibert Kayombo, WAMJW - MWANZA

Watumishi wa kada ya afya nchini wameaswa kuhakikisha wanadhibiti vifo vitokanavyo na uzazi na watoto wachanga kwa kuwajibika ipasavyo wakiwa kazini na kuepukana na tabia za uzembe.

Kauli hiyo imetolewa na na Mkurugenzi wa Huduma za Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe kutoka Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Dkt. Ntuli Kapologwe alipokuwa akizungumza na timu ya afya ya Mkoa wa Mwanza kwenye kikao kazi cha kujadili vifo vitokanavyo na uzazi na watoto wachanga kwa mkoa huo.

“Suala la vifo, pasipokuwepo na uwajibikaji na umoja ni vigumu sana kuweza kulifanikisha, kuchukua hatua imekuwa changamoto kwa timu nyingi hivyo kupelea kuongezeka kwa vifo” amesema Dkt. Ntuli.

Ameendelea kusema kuwa wataalam wa afya hawatakiwi kuoneana aibu endapo mjumbe wa timu hatofanya kazi yake ipasavyo kwa uzembe wake mwenyewe achukuliwe hatua za kinidhamu ili kuweza kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na kupunguza vifo vya akina mama na watoto wachanga.

Amesema kuwa wataalam wa afya wanapaswa kuwa wamoja na kushirikiana kikamilifu wakiwa kazini na kuacha kusubiri wataalam kutoka ngazi ya juu kuja kutoa maamuzi ya vitu ambavyo vingewezwa kufanywa na viongozi katika eneo husika.

Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza Bw. Emmanuel Tutuba amesema vifo vitokanavyo na uzazi na watoto wachanga vimekuwa viongezeka mkoani humo na kuwataka watumishi wa kada ya afya kuhakikisha wanapunguza kiwango cha vifo hivyo kwa mkoa huo ambao ni kinara wa huduma bora za afya katika Kanda ya Ziwa.

Akitaja takwimu za vifo hivyo, Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza Bw. Tutuba amesema katika kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2015 vifo vilikuwa 145, mwaka 2016 vifo 151, mwaka 2017 vifo 193, mwaka 2018 vifo 151, mwaka 2019 vifo 171 na kwa mwaka huu mpaka kufikia mwezi Septemba vimetokea vifo 142.

“Lazima tukae tutafakari, licha ya uwekezaji mkubwa ambao Serikali imefanya lakini vifo vinaongezeka, tunapokutana hivi tusiishie tuu kupashiana, ni lazima tutimize wajibu wetu” amesisitiza Bw. Tutuba.

Hata hivyo Bw. Tutuba amepongeza watumishi wa kada ya afya mkoani humo kwa juhudi zao wanazofanya kuhakikisha wanaokoa maisha ya watanzania pamoja na raia wa kigeni wanaokuja mkoani humo kwa ajili ya huduma za matibabu.

“Tumejitahidi kufanya mazuri mengi, lakini badi hatujatekeleza kwa asilimia 100, tumefanya vizuri lakini bado tungeweza kufanya vizuri zaidi endapo kila mmoja angetimiza wajibu wake” amesema Bw. Tutuba.

Mwisho



Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa akihutubia Wananchi kwenye maadhimisho ya siku ya Ukimwi Duniani yaliyofanyika katika uwanja wa Mandela Moshi, Mkoani Kilimanjaro yenye kauli mbiu ya "Mshikamano wa Kimataifa, Tujumuike Pamoja".

Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Prof. Mabula Mchembe akitoa taarifa ya hali ya maambukizi ya virusi vya UKIMWI mbele ya mgeni rasmi (Hayupo kwenye picha) wakati wa maadhimisho ya siku ya Ukimwi Duniani yaliyofanyika katika uwanja wa Mandela Moshi, Mkoani Kilimanjaro.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa akiteta jambo na Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Prof. Mabula Mchembe wakati wa maadhimisho ya siku ya Ukimwi Duniani yaliyofanyika katika uwanja wa Mandela Moshi, Mkoani Kilimanjaro. 

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa akipeana mkono na Mkurugenzi wa TACAIDS Dkt. leonard Maboko baada ya kuhutubia wananchi, wakati wa maadhimisho ya siku ya Ukimwi Duniani yaliyofanyika katika uwanja wa Mandela Moshi, Mkoani Kilimanjaro. 
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa akipata taarifa kutoka kwa Mkuu wa kitengo cha tiba na matunzo Dkt. Anath Rwebemberwa katika banda la Mpango wa Taifa wa kupambana na UKIMWI (NACP) ulio chini ya Wizara ya Afya, maendeleo ya jamii, jinsia, Wazee na watoto.

Picha ya pamoja ikiongozwa na Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Prof. Mabula Mchembe na Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Abel Makubi wakiwa na Mkurugenzi wa Kinga Wizara ya Afya Dkt. Leonard Subi (watano kutoka kushoto) Meneja NACP Dkt. Beatrecy Mutayoba (wamwisho), wakwanza kushoto ni Mkuu wa kitengo cha tiba na matunzo Dkt. Anath Rwebemberwa na wapili kushoto ni Mkuu wa kitengo cha Kinga (NACP) Dkt. Magreth Kagashe.


Picha ya pamoja ikiongozwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa akiwa na viongozi wengine Wakiserikali, wakati wa maadhimisho ya siku ya Ukimwi Duniani yaliyofanyika katika uwanja wa Mandela Moshi, Mkoani Kilimanjaro yenye kauli mbiu ya "Mshikamano wa Kimataifa, Tujumuike Pamoja".


WANAOFANYA MAPENZI NA WASICHANA WENYE UMRI MDOGO WAONYWA. 

Na Rayson Mwaisemba WAMJW- Kilimanjaro 

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa ametoa onyo kali kwa wanaofanya mapenzi (ngono) na wasichana wenye umri mdogo, hali inayosababisha kuwaharibia malengo yao ya baadae. 

Mhe. Kassim Majaliwa ameyasema hayo leo wakati akiwahutubia wananchi kwenye maadhimisho ya siku ya Ukimwi Duniani yaliyofanyika katika uwanja wa Mandela Moshi, Mkoani Kilimanjaro yenye kauli mbiu ya "Mshikamano wa Kimataifa, Tujumuike Pamoja".

"Nataka niwakumbushe na kutoa tahadhari kwa wale watu wazima mnaofanya mapenzi na vijana wadogo wa kike, ole wenu, ole wenu, ole wenu " ameyasema Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa.
Alisema kuwa, takwimu za maambukizi mapya ya VVU zinaonesha kwamba asilimia 40 ya maambukizi hutokea kwa vijana na katika hao asilimia 80 ni vijana wa kike, huku akiweka wazi kuwa, vijana ni kundi linalokabiliwa na changamoto ya maambukizi mapya ya VVU nchini.

Aliendelea kusema, kundi la vijana na hasa wa kike lipo kwenye hatari kubwa zaidi ya kupata maambukizi mapya, huku akidai uchambuzi wa kimazingira kuhusu takwimu hizi unaonesha kuwa sababu za vijana kuwa katika hatari ya maambukizi mapya ya VVU ni pamoja na kuanza ngono katika umri mdogo, vijana wadogo wa kike kuwa na mahusiano ya kingono na wanaume wenye umri mkubwa Matumizi yasiyo sahihi na endelevu ya mipira ya kike na kiume.

Aidha, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, ametoa wito kwa vijana kujitambua na kuthamini maisha yao kwa kujikinga na maambukizi mapya ya VVU, huku akiwakumbusha kuwa vijana ndio nguvu kazi ya Taifa, na kuwataka wale wanaoishi na VVU waendelee kutumia dawa za ARV kwa ufuasi sahihi bila kuacha ili kufubaza VVU na kuimarisha afya zao. 

"Natoa wito kwa vijana kujitambua na kuthamini maisha yao kwa kujikinga na maambukizi mapya ya VVU kwa kuwa ninyi ni nguvu kazi na Taifa linawategemea. Na wale wanaoishi na VVU waendelee kutumia dawa za ARV kwa ufuasi sahihi bila kuacha ili kufubaza VVU na kuimarisha afya zao", alisema Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa. 

Nae Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Prof. Mabula Mchembe amesema kuwa, Tanzania na Dunia kwa ujumla imepiga hatua kubwa katika jitihada za kukabiliana na janga la VVU na UKIMWI.

Aliendelea kusema kuwa, kama nchi inavyoelekea kufikia malengo ya Tisini Tatu, changamoto, na vipaumbele vimeendelea kubadilika kutokana na mafanikio ya mwitikio wa mapambano.
Takwimu zinaonesha kuwa wanaume, watoto, vijana wanaopevuka na vijana wadogo, na watu wanaofanya tabia hatarishi, wako nyuma kutambua hali zao, ufuasi hafifu wa tiba, na ufubazaji wa VVU usioridhisha. 

Hata hivyo, Prof. Mabula Mchembe amesema kuwa, Serikali inaendelea na jukumu la kutafiti, kuandika na kusambaza taarifa za kitaalamu zinazochambua na kutoa masuluhisho ya changamoto zitazotumika kuhuisha sera, miongozo na taratibu za huduma na afua za VVU na UKIMWI. 

"Tunalo jukumu sasa, la kutafiti, kuandika na kusambaza taarifa za kitaalamu zinazochambua na kutoa masuluhisho ya changamoto hizi ili sasa yatumike kuhuisha sera, miongozo na taratibu za huduma na afua za VVU na UKIMWI", amesema Prof. Mchembe 

Mwisho.


MKRdezign

{facebook#YOUR_SOCIAL_PROFILE_URL} {twitter#YOUR_SOCIAL_PROFILE_URL} {google-plus#YOUR_SOCIAL_PROFILE_URL} {youtube#YOUR_SOCIAL_PROFILE_URL} {instagram#YOUR_SOCIAL_PROFILE_URL}

Contact Form

Name

Email *

Message *

Powered by Blogger.
Javascript DisablePlease Enable Javascript To See All Widget