Latest Post

Mkurugenzi Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Grace Magembe akiwasalimia wagonjwa waliokuwa wakisubiri huduma katika eneo la wagonjwa wa nje (OPD) katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara.

Mkurugenzi wa tiba Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Grace Magembe akimjulia hali moja kati ya wagonjwa waliofika kupata huduma za Afya katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara, pindi alipofanya ziara katika Hospitali hiyo.
Mkurugenzi Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Grace Magembe (wa katikati) akiwa pamoja na  Mkurugenzi wa uhakiki ubora wa huduma kutoka Wizara ya Afya Dkt.  Eliakim Eliud wakikagua muongozo  wa utoaji huduma kwa kwa Wauguzi, pindi walipofanya ziara ya kukagua hali ya utoaji huduma za Afya katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara.


Mkurugenzi Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Grace Magembe akiwa na Wataalamu wa Maabara katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara.
 
Mkurugenzi wa tiba Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Grace Magembe akiwa na Wataalamu wa Maabara katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara,  wakati alipofanya ziara ya kukagua hali ya utoaji huduma za Afya katika Hospitali hiyo.

Mkurugenzi Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Grace Magembe akikagua kadi inayoonesha hali ya idadi ya dawa zilizopo (Bin Card) katika chumba cha kuhifadhia dawa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara.

 

WATOA HUDUMA WATAKIWA KUFANYA KAZI KWA WELEDI KWA KUZINGATIA MAADILI.

Na Rayson Mwaisemba, WAMJW- MANYARA

MKURUGENZI wa tiba Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Grace Magembe ametoa wito kwa Watoa huduma za Afya nchini kufanya kazi kwa weledi kwa kuzingatia maadili wakati wa kumhudumia mgonjwa.

Dkt. Grace Magembe ametoa rai hiyo leo, wakati alipofanya ziara ya kukagua hali ya utoaji huduma za afya, na ujenzi wa miundombinu katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara.

Dkt. Grace amesema kuwa, kwa kiasi kikubwa Serikali imewekeza kwenye ujenzi wa miundombinu, vifaa tiba na hali ya upatikanaji wa dawa, ikiwa ni sehemu ya maboresho ya utoaji huduma za afya bora kwa mwananchi katika jamii.

"Serikali imewekeza kwenye miundombinu, kwenye vifaa tiba, hali ya upatikanaji wa dawa, lakini Watumishi wanatakiwa wafanye kazi kwa weledi kwa kuzingatia maadili ya kazi zao wakati wa kumuhudumia mgonjwa " alisema Dkt. Grace.

Aliendelea kusema kuwa, Serikali imekuwa ikisisitiza sana, kuhusu maadili mazuri wakati wa utoaji huduma kwa wateja, pindi wanapokuja kupata huduma, hii inajumuhisha mapokezi yake, muda anaotumia kusubiri huduma, muda wa kurejesha majibu yake na kauli zinazotumika wakati wa utoaji huduma.

Hata hivyo, Dkt. Grace ametoa wito kwa viongozi wa hospitali kuwa na mpango madhubuti wa matengenezo ya vifaa tiba ili kuepuka ewezekano wa kusimama kwa baadhi ya huduma, hali itayopelekea wananchi kukosa huduma na upotevu wa mapato.

"Kitu kingine ambacho tunasisitiza katika hospitali ni kuwa na mpango madhubuti wa matengenezo ya vifaa tiba, vifaa ambavyo vimenunuliwa na Serikali ni vya gharama kubwa mnoo, fedha nyingi sana zimetumika, kwahiyo tunasisitiza kuwa na mpango wa matengenezo" alisema

Aidha, Dkt. Grace kwa kiasi kikubwa ameridhishwa na hali ya upatikanaji wa dawa katika maeneo alipofanya ziara, huku akitoa rai kwa Watoa huduma kuhakikisha mgonjwa anapoandikiwa dawa azipate dawa alizoandikiwa lakini pia azipate kwa kwa muda sahihi.

" tumeangalia tena suala la upatikanaji wa dawa, namna dawa inavyohifadhiwa, namna dawa inavyotumika, namna dawa inavyotoka chumba cha kuhifadhia mpaka inapomkuta mhitaji wodini, hii yote tumeifanyia kazi kwasababu tunataka hizo dawa zitumike kulingana na mahitaji yaliyotakiwa" alisema Dkt Grace.

Mbali na hayo, Dkt. Grace amesisitiza agizo la Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Abel Makubi juu ya kufanya kazi kwa juhudi na ushirikiano ili kupunguza vifo vya mama na mtoto, huku akisisitiza kuwa, kuweka mikakati thabiti katika mapambano dhidi ya vita hii, na kuweka wazi kuwa vifo vya mama na mtoto vitakuwa ni kigezo cha kuangalia uwajibikaji na utendaji kazi wa Waganga Wakuu wa Mikoa, Wilaya na Waganga wafawidhi.

"Hatutaki kuona mama wa Kitanzania anakufa wakati analeta kiumbe Duniani, vifo vingi vinasababishwa na sababu ambazo zinaweza kuzuilika, lazima kila Mtumishi afanye kazi, kuanzia Mganga Mkuu wa Mkoa, Mganga Mkuu wa Wilaya, hospitali zote zilizopo ndani ya Mkoa wake, wote wafanye kazi kwa kushirikiana, wake na mkakati, sisi kama Wizara kwa kushirikiana na TAMISEMI tutaendelea kufuatilia tuone kama vifo vinapungua au la na hatua zitachukuliwa " alisema.

Nae, Mkurugenzi wa uhakiki ubora huduma Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Eliakim Eliud amesisitiza kuwa, kuongeza kazi za utoaji huduma kwa kuzingatia ubora wa huduma na kufuata miongozo ya kujikinga wakati wa kuwahudumia wagonjwa.

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Manyara Dkt. Damas Kayera ameweka wazi kuwa, Mkoa wa Manyara umeendelea kuwa ma rekodi nzuri juu ya hali ya upatikanaji wa dawa muhimu wa kufikia wastani wa 91%, jambo lililosaidia kupunguza malalamiko kwa wananchi wanaokuja kupata huduma.

"Mkoa unaendelea kuwa na rekodi nzuri ya ongezeko la dawa muhimu, zinazofuatiliwa na Wizara ya afya kwa kila kituo, ambapo kwa kipindi cha nusu mwaka 2020 kumekuwa na wastani wa 91%" amesema.

Mwisho.







Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto-Idara Kuu Afya Edward Mbanga akiongea na Wauguzi Wakuu wa Wilaya nchini wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha kuwajengea uwezo wa kusimamia maadili na utendaji kazi kwenye ukumbi wa Cathedral jijini Dodoma.

Kaimu Katibu Mkuu, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsai, wazee na Watoto akiongea na viongozi  hao wakati wa kikao cha mafunzo ambapo aliwataka kuweka dhamira na malengo  ya dhati  katika kuboresha maadili katika taaluma ya uuguzi na ukunga.

Muuguzi Mkuu kutoka Ofisi ya Rais-TAMISEMI Charles Kadugushi akiongea na Wauguzi Wakuu wa Wilaya nchini wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha kuwajengea uwezo wa kusimamia maadili na utendaji kazi, Jijini Dodoma.

Mkurugenzi wa Idara ya Uuguzi na Ukunga kutoka Wizara ya Afya Bi. Ziana Sellah akiongea na Wauguzi Wakuu wa Wilaya nchini wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha kuwajengea uwezo wa kusimamia maadili na utendaji kazi, Jijini Dodoma.

Msajili wa Baraz a la Uuguzi na Ukunga Agnes Mtawa akiwasilisha mada wakati wa kikao kazi hicho kinachofanyika jijini Dodoma.

Picha ya pamoja ya mgeni rasmi na wasajili wa mabaraza ya kitaaluma yaliyopo chini ya wizara ya afya.

Mgeni rasmi akiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya wauguzi wakuu wa Wilaya mara baada ya ufunguzi.


WAUGUZI NA WAKUNGA WATAKIWA KUTUMIA UTAALAMU WAO KWA AJILI YA USTAWI WA TAIFA

Na.Catherine Sungura,WAMJW-Dodoma

Wauguzi na Wakunga nchini wametakiwa kutoa huduma kwa kuzingatia miongozo iliyopo wakati wakitoa huduma kwa weledi ili kufikia malengo na matumaini ya wateja kwa ajili ya ustawi wa Taifa.

Rai hiyo imetolewa leo na Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto – Idara Kuu ya Afya Bw. Edward Mbanga wakati wa ufunguzi wa  kikao kazi  cha kuwajengea uwezo wa kusimamia maadili na utendaji kazi wauguzi wakuu wa wilaya kinachofanyika jijini Dodoma.

Bw. Mbanga amesema  kuwa wauguzi na wakunga ndio watendaji wakuu katika vituo vya afya kwenye ngazi ya jamii hadi Taifa hivyo uwajibikaji mzuri na utawala bora utaboresha utendaji hali itayosaidia kufikia malengo mbalimbali waliyojiwekea katika ngazi zote.

"Viongozi mnatakiwa kuwa wabunifu, wachapa kazi, wenye nidhamu na mfano bora wa kuigwa katika utekelezaji wa majukumu yenu,kwahiyo  ni lazima msimamie utoaji wa huduma uliyo mzuri na wenye heshima na utu.”Alisema

Aidha, Kaimu Katibu Mkuu huyo aliwakumbusha  washiriki hao kuwa, suala la huduma za uuguzi na ukunga ni suala la  ubinadamu zaidi na kuvaa viatu vya wagonjwa wao.

“Hakuna aliyegongwa muhuri wa kuugua  au kuwa mgonjwa akalazwa ,sisi sote ni wagonjwa watarajiwa kwahiyo kama ambavyo sisi tungependa kuuguzwa vizuri, kijibiwa kwa kauli nzuri basi tuhakikishe tunasimamia maadaili ya kazi”.Alisisitiza Mbanga.

Hatahivyo alisema kuwa, Serikali inawahakikishia itaendelea kufanya kazi pamoja na waauguzi  kwa kutoa miongozo thabiti na kuhakikisha upatikanaji wa nyenzo muhimu katika hospitali na vituo vya kutolea huduma ya afya na kuboresha mazingira ya kazi yaliyo bora na salama.

Aliendelea kusema kuwa, hivi karibuni kumekuwa na malalamko  mbalimbali ya kiutendaji  na kitaaluma kutoka kwa wateja  wanaofika kupata huduma za afya na hivyo kuleta taswira mbaya  kwa taaluma yao na kuonyesha hakuna usimamizi mzuri wa utoaji huduma za uuguzi na ukunga.

“Tungependa  wateja wetu watoe sifa  badala ya malalamiko hivyo kikao hiki mje na mipango ya kuondokana na malalamiko kwani taaluma yenu ni zaidi taaluma." alisema.

Hata hivyo, amewakumbusha  viongozi hao kuwa mstari wa mbele kupambana dhidi  ya rushwa na kuhakikisha inatokomezwa katika maeneo yao ya kazi kwani rushwa imekuwa ikilalamikiwa na kuripotiwa katika kada ya afya nchini.

-MWISHO-





Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Abel Makubi akikagua wodi ya wanaume iliyoko hospitali ya rufaa ya mkoa Dodoma.Kushoto ni Muuguzi Mfawidhi wa hospitali hiyo Stanley Mahumbo.

Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Abel Makubi akikagua duka la dawa la Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.
Mganga Mkuu wa Serikali akitazama moja ya faili la   mgonjwa aliolazwa kwenye wodi hiyo ambapo alibaini mapungufu.

Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Abel Makubi akiangalia moja ya mashine zilizopo kwenye maabara ya hospitali hiyo.

Na. WAMJW-Dodoma

Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Abel Makubi ameuagiza Uongozi wa  Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma kuboresha huduma za tiba kwa wananchi wanaofika kupata huduma za afya katika hospitali hiyo.

Prof. Makubi ametoa maagizo hayo kufuatia ziara ya kushtukiza aliyoifanya kwenye Hospitali hiyo na kushuhudia changamoto mbalimbali ikiwemo baadhi ya wagonjwa kuchelewa kupewa huduma, Madaktari bingwa kutowaona wagonjwa kwa wakati na huduma za vipimo kuchelewa.

“Yapo mazuri tumeona mnayofanya kwa wananchi na tunawapongeza, ila lazima kuangalia upande wa pili ambao wananchi wanayataka, kwa yale mapungufu tuliyoyaona tungependa kuona yanaboreshwa haraka ili hospitali hii iwe ya mfano kwa hospitali zote za rufaa za mikoa kwa kutoa huduma zilizo bora”.

Prof. Makubi amesema hospitali hiyo inatakiwa kuonesha mfano kuanzia utoaji wa huduma bora kwa mteja pamoja, kupunguza muda wa wagonjwa kusubiri huduma, upatikanaji wa wauguzi na mabingwa wanapohitajika na usafi wa wodi kwani ndiyo chachu ya wananchi wengi kufika hapo na kupata huduma kabla hawajapewa rufaa ya kwenda Hospitali kubwa kama Benjamin Mkapa.

Aidha, Mganga Mkuu huyo ameutaka uongozi na watumishi wa hospitali hiyo kutambua majukumu yao  kwa kuonesha kuwajali wananchi  wote na kuwataka kuweka utaratibu usio na usumbufu kwa wagonjwa na kupatiwa huduma kwa wakati.

Prof. Makubi alionyesha kusikitishwa alipokuta wodini  baadhi ya wagonjwa wamelazwa na hawajaonwa na Mabingwa kwa zaidi ya siku tatu, wauguzi wakiwa hawajaambatana na madaktari katika kuzungukia wagonjwa huku madaktari wa vitendo (interns)  wakifanya “procedures” peke yao bila uangalizi na baadhi ya  wagonjwa wengine wakiwa wamelazwa chini wakati vitanda viko wazi pamoja na mazingira ya wodi hayakuwa ya kuridhisha na kukosekana kwa mpangilio wa vifaa (5S)

 “Lazima watumishi mjitambue mko wapi kwani awamu hii ni ya kuwajali wanyonge na kufanya kazi  kwa bidii ndio kanuni ya awamu hii hapa kazi tu”. Alisisitiza Prof. Makubi.

Prof. Makubi ameelekeza madaktari wa hospitali hiyo kufanya kazi kwa ushirikiano na wauguzi katika kuwahudumia wagonjwa katika wodi, kuleta mabadiliko kwa kutengeneza miongozo mbalimbali ya kusimamia huduma na kuacha kufanya kazi kwa mazoea ili kila mwananchi anayefika hospitalini hapo ahudumiwe kwa wakati na huduma inayostahili.

Kwa upande mwingine Mganga Mkuu huyo wa Serikali ameitaka hospitali hiyo kuboresha idara ya huduma kwa wateja (Customer Care) kwani hakuna mgonjwa anayependa kuchelewa kupata huduma hivyo lazima kutoa huduma bora na zinazohitajika kwa wananchi wote.

Prof. Makubi ameelekeza Uongozi wa Hospitali kuhakikisha mashine za maabara ambazo zimeishiwa vitendanishi, zinaanza kufanya kazi haraka.

"Ni vizuri mkapunguza muda wa kusubiri majibu ya vipimo vya damu, X-ray, ultrasound, na Moyo na vipimo vingine".Alielekeza Prof. Abel Makubi.

Prof. Makubi aliagiza Hospitali zote nchini zifanyie kazi changamoto alizoziona hapo Dodoma, na akaagiza Idara ya ukaguzi wa huduma bora kutoka wizarani wafanye ufuatiliaji wa utoaji wa huduma mikoani,  wilayani na Vituo vya afya kila mwezi na kutoa taarifa kwake.


Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Abel Makubi akiongea na wataalam kutoka Wizara ya Afya na TAMISEMI wakati wa kujadili utoaji wa huduma bora za afya kwenye vituo vya afya,hospitali za halmashauri na rufaa zilizojengwa kukarabatiwa na Serikali
Mkurugenzi wa huduma za Afya, Lishe na Ustawi wa Jamii-TAMISEMI Dkt. Ntuli Kapologwe akiongea wakati wa kikao hicho.
Mkurugenzi wa Idara ya Kinga kutoka Wizara ya Afya Dkt. Leonard Subi akiwasilisha mada wakati wa kikao baina ya Wizara ya Afya na TAMISEMI






Na. WAMJW-Dodoma

Serikali imefanikiwa kutimiza dhamira ya kuhakikisha kunakuwa na upatikanaji na uwiano wa kutosha katika utoaji huduma za afya pamoja na kuhakikisha wananchi wanapata huduma za afya za uhakika na wakati.

Hayo yamesemwa leo na Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Abel Makubi wakati akifungua kikao kati ya Wizara ya Afya na Ofisi ya Rais-TAMISEMI cha kujadili utoaji huduma bora za afya kwenye vituo vya afya, Hospitali za Halmashauri na Rufaa zilizojengwa na kukarabatiwa na serikali ya awamu ya tano.

“Sisi kama wataalam tunawajibu wa kuendeleza chachu ya maendeleo  yaliyofikiwa na kuhakikisha vituo hivi vinafunguliwa kwa kuzingatia utaratibu unaotakiwa na kuendelea kutoa huduma vikiwa na vifaa vyote muhimu na wataalam wenye weledi na stadi katika kupambana na magonjwa na kupunguza vifo vinavyozuilika”.Amesema Prof. Makubi.

Prof. Makubi ameongeza kuwa mafanikio hayo yamepatikana kufuatia sekta ya afya kuchukua jukumu la kufanya ukarabati wa ujenzi katika vituo vya kutolea huduma za afya ambapo iliweka kipaumbele kwenye vituo vya afya vya msingi ili kuviwezesha kutoa huduma za dharura za uzazi na mtoto mchanga.

“Tumejenga hospitali mpya za wilaya 99, kutoka hospitali 70 za awamu ya kwanza zimekamilika na nyingi zimeanza kutoa huduma hata hivyo serikali imeongeza kujenga hospitali nyingine 29 na fedha zake zimetengwa tayari”. Ameongeza Prof. Makubi.

Awali akiongea kwa niaba ya Naibu katibu Mkuu wa Afya TAMISEMI, Mkurugenzi wa huduma za Afya, Lishe na ustawi wa jamii Dkt. Ntuli Kapologwe amesema kuwa kikao hicho kina lengo la kuwa na muelekeo mzuri wa sekta ya afya hivyo ushirikiano wa pamoja kati ya Wizara hizo mbili ni muhimu katika kufanikisha na kusukuma mbele sekta hiyo nchini.

Naye Mkurugenzi wa huduma za kinga kutoka Wizara ya Afya Dkt. Leonard Subi amesema kuwa vituo vya afya 570 vilivyojengwa na kukarabatiwa na Serikali vimeweza kuboresha huduma za afya na kuzuia vifo vya akina mama wajawazito na watoto wachanga huku vikiwa na uwezo wa kutoa huduma za dharura kama upasuaji.

MWISHO

Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu akiongozana na Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Bw. Gelasius Byakanwa wakikagua ujenzi wa Hospitali mpya ya kanda ya kusini inayojengwa Mkoani Mtwara.

Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu akisikiliza maelezo kutoka kwa msanifu majengo anayesimamia mradi wa ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya kanda ya kusini wakati alipotembelea Hospitali hiyo kuona hali ya ujenzi.

Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu akiwa na Mbunge wa Mtwara vijijini Mhe. Hawa Ghasia wakitembelea ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya kanda ya kusini iliyopo Mtwara.


Sehemu ya jengo la Hospitali ya Rufaa ya Mikoa ya kusini inayoendelea na ujenzi.

Na. WAJMW-Mtwara

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu ametembelea ujenzi wa Hospitali mpya ya Rufaa ya Mikoa ya kusini iliyopo mkoani Mtwara na kuridhishwa na kasi ya ujenzi wa Hospitali hiyo.

Waziri Ummy ameonekana kuridhidhishwa na ujenzi wa Hospitali hiyo ambao umefikia asilimia 80 na inagharimu Shilingi Bilioni 15.8 mpaka kukamilika kwake.

"Kukamilika kwa Hospitali hii kutasaidia kupunguza rufaa kwa wananchi wa mikoa ya kusini kwenda kutafuta huduma za kibingwa Muhimbili, MOI au JKCI, huduma zote zitakua zinapatikana hapa". Amesema Waziri Ummy.

Waziri Ummy amesema lengo la Wizara ya Afya ni kuona huduma zinaanza kutolewa katika Hospitali hiyo kabla ya kuanza kampeni za uchaguzi mwaka huu kwani ilikua ni ahadi ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli alipopita mwaka 2015 kuomba kura na Hospitali hiyo ipo kwenye utekelezaji wa ilani ya Chama cha Mapinduzi.

"Hatutaki watu wa Mtwara na mikoa ya kusini kwa ujumla muende Dar Es Salaam kwa ajili ya kufuata huduma za CT-Scan, huduma za madaktari bingwa ikiwemo upasuaji wa mifupa, mishipa ya fahamu, Madaktari wa watoto na uzazi. Huduma zote hizi zitapatikana hapa mara baada ya ujenzi wa Hospitali hii kukamilika". Amesema Waziri Ummy.

Waziri Ummy amesema kwa ujumla hali ya sekta ya Afya mkoani Mtwara ni nzuri ambapo katika kipindi cha miaka mitano Hospitali mpya za Wilaya tatu zimejengwa ambazo ni Nanguluwe, Nanyamba pamoja na Masasi. Aidha, vituo vya Afya vinane vimejengwa katika Mkoa huo katika kipindi hicho na kufanya idadi kufikia vituo 23 kutoka 15 wakati Rais Magufuli anaingia madarakani.

MKRdezign

{facebook#YOUR_SOCIAL_PROFILE_URL} {twitter#YOUR_SOCIAL_PROFILE_URL} {google-plus#YOUR_SOCIAL_PROFILE_URL} {youtube#YOUR_SOCIAL_PROFILE_URL} {instagram#YOUR_SOCIAL_PROFILE_URL}

Contact Form

Name

Email *

Message *

Powered by Blogger.
Javascript DisablePlease Enable Javascript To See All Widget