Latest Post



Na. Catherine Sungura, WAMJW-Dodoma

Serikali  imeweza kujibu changamoto za kuwahudumia wananchi  kwa kuimarisha  huduma za afya ya dharura  kwa kusimika  mitambo ya kufua  hewa tiba (Oksijeni) na hivyo kupunguza gharama za uendeshaji wa hospitali za rufaa za mikoa nchini.

Hayo yamesemwa leo na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima wakati alipotembelea hospitali ya rufaa ya mkoa Dodoma kujionea jinsi walivyounganisha mitambo hiyo kwenye wodi ya wagonjwa mahututi  na  watoto.

Dkt.Gwajima amesema mitambo hiyo ambayo Serikali kwa kushirikiana na Benki Kuu ya Dunia hivi sasa imefungwa kwenye hospitali za rufaa za mikoa saba ya Dodoma, Mtwara ,Manyara, Mbeya, Amana Geita na Songea na hivyo wizara yake ipo njiani kukamilisha kufungia hospitali zote za rufaa za mikoa hapa nchini.

“Mitambo hii  imefungwa kwa gharama  isiyopungua bilioni 1.4 kila hospitali na inalenga kuzalisha mitungi 200 ya hewa hiyo kwa masaa 24 , na kila mtambo unayo sehemu  ya mabomba yenye mita 400 yanayosafirisha hewa hii pia mitungi 73 imenunuliwa pamoja na mitambo hii kwa hila hospitali haya ni mapinduzi makubwa”. Alisisitiza.

Aidha, Dkt. Gwajima amefurahishwa na uongozi wa hospitali hiyo kwa kukamilisha kufunga  mitambo hiyo  na kuanza kutoa huduma kwenye wodi ya wagonjwa mahututi(ICU) pamoja na wodi ya watoto na hivyo wameweza  kuunganisha vitanda 78 kutoka vitanda 10 vya awali na kufanya jumla ya vitanda 88 kupatiwa huduma hiyo hospitalini hapo.

“Hatua hii itapunguza  kwa kiwango kikubwa  gharama za  kuhudumia mgonjwa  mwenye mahitaji ya hewa hii,wito wangu  tuitumie vizuri na kuzingatia na kuhakikisha  matengenezo kinga  yanafanyika kwa ufanisi”.

Dkt. Gwajima amesema kuwa uwekezaji huo umeweza kujibu changamoto  ya kipindi cha mlipuko wa Covid-19 ulioripotiwa  nchin mwezi Machi mwaka 2020 na hivyo kusababisha kuongezeka kwa mahitaji ya hewa ya oksijeni na kuwa gharama zake zilipanda.

“Niwapongeze sana waganga wafawidhi wa hospitali za rufaa za mikoa kwa kuja na wazo hili la kufunga mitambo hiyo kwenye hospitali zetu na hivyo tutaweza kusaidia hospitali za wilaya na vituo vya afya na hivyo kuwapunguzia matumizi ya fedha ya kununua oksejeni ,haya ni mapinduzi makubwa kwa Serikali yetu”. Alisisitiza Dkt. Gwajima

Aliongeza kuwa Kwa upande kwa kuepuka magonjwa ya kuambukiza ambayo  yameanza kuyakumba mataifa mengine, Waziri huyo aliwataka waganga wakuu wa mikoa na wafawidhi kwenye hospitali za rufaa za mikoa kuendelea kutoa elimu kwa umma kwa kutumia vyombo vya radio vilivyopo kwenye maeneo yao (Community radio) ili kuwaondolea wananchi hofu na kuendelea kuchukua tahadhari ya kujikinga na magonjwa ya kuambukiza na yasiyoambukiza ikiwemo janga la Corona.

“Serikali kupitia sekta ya afya  kwa kushirikia na wadau wake nchini iko makini  kufuatilia kinachoendela duniani na kuchukua  hatua mbalimbali  za kuhakikisha nchi yetu  inaendelea kuwa salama na imara  katika kudhibiti  milipuko ya magonjwa  mbalimbali ikiwemo  huu wa Covid-19”.Alisema Dkt. Gwajima.

Dkt. Gwajima aliwakumbusha wadau,wataalam pamoja na wananchi wote kuendelea kuchukua  tahadhari muhimu ambazo zimekuwa  zikielemishwa mara kwa mara  dhidi ya kujikinga  na kudhibiti magonjwa mbalimbali ikiwemo C0vid-19 kwa kuepuka hofu,kuimarisha tabia  ya kunawa mikono mara kwa mara  kwa maji safi tiririka na sabuni,kufanya mazoezi,kula lishe  au vyakula vya mbogamboga kwa wingi na matunda,kutumia tiba asili, kuepuka misongamano isiyo ya lazima  na mwisho kuwahi kwenye vituo vya kutolea huduma za afya  mara unapoona dalili za maradhi yeyote.

Naye Mganga Mfawidhi wa hospitali ya rufaa ya mkoa Dodoma Dkt. Ernest Ibenzi amesema  wanatarajia kufunga mitambo  ya kujazia hewa tiba hiyo ili kuweza kusaidia vituo vya afya vilivyo jirani na kusambaza huduma hiyo kwenye hospitali nzima.

-Mwisho-



Prof. Abek Makubi Katibu Mkuu Wizara ya Afya






Na. WAMJW - Dodoma. 

Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imeanza kutekeleza kwa kasi maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ikiwa ni sehemu ya maboresho ya utoaji huduma katika Sekta ya Afya.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu Wizara ya Afya - Idara Kuu Afya Prof. Abel Makubi katika kikao na Watumishi wa Idara Kuu ya Afya Makao Makuu kilichofanyika katika ukumbi wa Hazina Jijini Dodoma.

Katika kutekeleza maagizo hayo Prof. Makubi amesema kuwa, Wizara inategemea kuwasilisha Bungeni mchakato wa kuridhiwa kwa Bima ya Afya kwa wote ili uweze kupitishwa na kuwezesha wananchi wote kuwa na Bima ya Afya hali itakayosaidia kupunguza gharama za matibabu kwa wananchi wote.

"80% ya Watanzania ni watoto wa wakulima, Wizara imepeleka mchakato huu haraka bungeni ili uweze kupitishwa, ambapo utasaidia wananchi wote kuwa na Bima ya Afya, jambo litalosaidia kupunguza gharama za matibabu kwa wananchi," amesema Prof. Makubi. 

Aliendelea kusema kuwa, Serikali inaendelea kuweka mikakati mizuri itayosaidia wananchi ambao hawatakuwa na uwezo wa kulipa kiasi hicho ili kupata Bima ya Afya kwa kutafuta vyanzo vingine vya fedha ili kuwalipia huduma hiyo.

Hata hivyo, Prof. Makubi amesema kuwa, katika miaka mitano iliyopita Serikali imejenga vituo vya kutolea huduma za Afya vya kutosha ikiwemo Hospitali za Kanda, Hospitali za Wilaya, Hospitali za Rufaa za Mikoa, Vituo vya Afya na Zahanati, na hivyo katika kutekeleza agizo hilo amesema Wizara inaendelea kuhakikisha maboma yote yanakamilika na kuanza kutoa huduma za Afya kwa wananchi kwa kiasi kidogo cha fedha ndani ya miundombinu yenye ubora.

Kwa upande mwingine amesema kuwa, licha ya malalamiko kutoka kwa wananchi juu ya hali ya upatikanaji wa dawa kutoridhisha nchini, Wizara ya imepokea jumla ya Tzs.Bilioni 80 kutoka Serikalini ili kuboresha hali ya upatikanaji wa dawa kwa wananchi. Ameonya kuwa Serikalini haitakubali kuona fedha hizi zinatumiwa vibaya au dawa kuibiwa katika vituo vya kutolea huduma. 

Aliendelea kusema kuwa, katika kuimarisha zaidi eneo hilo, Wizara imekutana na Wazabuni ili kuendelea kuimarisha hali ya upatikanaji wa dawa, jambo litalosaidia kupunguza changamoto za malalamiko yanayotokana na ufinyu wa huduma za dawa katika vituo vya kutolea huduma. 

Kuhusu masilahi ya watumishi, Profesa Makubi alisisitiza maelekezo ya Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan kuhakikisha “motivations” zinatolewa , hasa kwa kazi nzuri zinazofanyika. Ameelekeza Taasisi zote chini ya Sekta ya Afya kwa moyo wa shukurani na pongezi kwa watumishi wanaojituma kupitia haki zao, mapato ya ndani, na miradi mbalimbali pale ambapo miongozo inaruhusu .

Aidha, Prof. Makubi amesema kuwa, moja kati ya kipaumbele cha Wizara ya Afya ni kupunguza vifo vya mama na mtoto wakati wa kuleta kiumbe kipya Duniani, hivyo kuwataka Watumishi wa Wizara ya Afya kwa kushirikiana na OR TAMISEMI kusimamia huduma bora ili kupunguza vifo hivyo ikiwezekana kuviondoa kabisa.

"Ni wajibu wetu kupunguza vifo vya mama na mtoto, naomba hili tulisimamie wote, nisingependa kuona vifo vya mama, wakati analeta kiumbe kipya Duniani," alisema Prof. Abel Makubi. 

Kwa upande mwingine, Prof. Makubi amesema kuwa, Wizara imeendelea kuhamasisha wananchi kushiriki katika mapambano dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza kwa kuboresha mtindo wa maisha ikiwemo kufanya mazoezi, kula mlo unaofaa na kupata elimu juu ya kujikinga dhidi ya magonjwa hayo.

Aliendelea kwa kutoa maelekezo ya kuongeza kasi katika kutoa elimu kwa wananchi hususan watoto ili kujenga tabia ya kupenda kufanya mazoezi na kufuata mlo kamili, huku akiwaasa Watumishi wa Afya kuwa mstari wa mbele kwa kufanya mazoezi na kutoa elimu kwa wananchi. 

Aliendelea kwa kuwapongeza Watumishi wote wa Sekta ya Afya kwa namna walivyoshiriki katika mapambano dhidi ya magonjwa ya kuambukiza ikiwemo magonjwa ya mlipuko kama vile ugonjwa wa Corona, huku akiwataka kuendelea kujikinga dhidi ya ugonjwa huo kwa kuchukua tahadhari zote muhimu kama kunawa mikono kwa sabuni na maji safi yanayotiririka, kuvaa barakoa pale panapohitajika na kuepuka msongamano isiyo ya ulazima.

Hata hivyo, Prof. Makubi amesisitiza juu ya kuongeza kasi katika kuboresha huduma za tiba asili, huku akielekeza kuwa na kituo cha Kisasa cha Tiba Asili kitachorahisisha shughuli zote ikiwemo tafiti kuhusu tiba asili na kuweka wazi kuwa dawa za tiba asili ziweze kupatikana katika maduka ya dawa (famasi).

Huduma kwa wateja, ni sehemu nyingine ambayo Prof. Makubi amesisitiza iongeze kasi kwa Watumishi, huku akielekeza Huduma kwa Wateja (Customer Care) zianze kutolewa kwa wateja mara wanapoingia getini au mlango mkuu mpaka wanapomaliza kupokea huduma na kuondoka. 

"Huduma nzuri kwa wateja zianze kwetu ndani ya Wizara, wageni wapokelewe vizuri kuanzia getini, hatupendi kusikia malalamiko ya watu hawajapokelewa vizuri, wote tuna nafasi ya kupokea na kuwasikiliza wateja pindi wanapokuja kuhitaji huduma," amesema. 

Pia, Prof. Makubi ameagiza kuongezeka kwa kasi ya kushughulikia kero kutoka kwa wananchi ili waweze kupata huduma kwa haraka, aliendelea kusema kuwa kila mtumishi kwa nafasi yake ahakikishe anashughulikia kero za wananchi ili zisifike ngazi ya viongozi wa juu.  

Mwisho.



 
Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa huduma za Maabara Dkt. Mathius Katura akifafanua jambo baada ya kufungua kikao cha Waratibu wa Maabara binafsi wa mikoa, kilichofanyika Mkoani Morogoro.
 
 
Msajili wa Maabara binafsi nchini Bw. Dominic Fwiling'afu akieleza jambo baada ya ufunguzi wa kikao cha Waratibu wa huduma za Maabara wa mikoa kilichofanyika Mkoani Morogoro.
 
 
Mratibu wa huduma za Maabara kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI Bw. Ferdinand Matata akieleza jambo baada ya ufunguzi wa kikao cha Waratibu wa huduma za Maabara wa mikoa kilichofanyika Mkoani Morogoro.
Msajili wa Maabara binafsi nchini Bw. Dominic Fwiling'afu akiongea jambo na Waratibu wa huduma  za Maabara wa mikoa baada ya ufunguzi wa kikao hicho kilichofanyika Mkoani Morogoro.
 
Baadhi ya Waratibu wa Maabara Mkoa wakifuatilia maelekezo kutoka kwa mgeni rasmi.
 
 
Waratibu wa huduma za Maabara wa mikoa wakiendelea kubadilishana mawazo na uzoefu katika kuwahudumia wananchi katika maeneo yao.
 
Picha ya pamoja ya Waratibu wa Maabara binafsi wa mikoa, baada ya ufunguzi wa kikao cha Waratibu wa huduma za Maabara wa Mikoa kilichofanyika Mkoani Morogoro.
 

 

WARATIBU WA MAABARA WAAGIZWA KUSIMAMIA UBORA WA HUDUMA KATIKA MAENEO YAO.

Na Mwandishi wetu - Morogoro

Waratibu wa huduma za Maabara ngazi zote nchini wameagizwa kusimamia utoaji huduma bora za Maabara kwa wananchi katika maeneo yao ili wagonjwa wapate tiba sahihi na kuondokana na malalamiko yanayojitokeza bila sababu ya msingi.

Rai hiyo imetolewa na Kaimu Mkurugenzi msaidizi wa huduma za Maabara Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Katura Mathius wakati wa ufunguzi wa kikao cha Waratibu wa Maabara ngazi ya Mkoa kilichofanyika Mkoani Morogoro.

Dkt. Katura amesema kuwa, Sheria na Kanuni namba 10 ya mwaka 1997 na miongozo ya Wizara ya Afya inawataka Waratibu wa huduma za Maabara ngazi ya Mkoa kusimamia uanzishwaji na utoaji huduma bora za Maabara binafsi ili wagonjwa wapate tiba sahihi.

"Waratibu wa huduma za Maabara ngazi ya Mkoa, mnalazimika kusimamia Sheria na Kanuni hii namba 10 ya mwaka 1997 na miongozo ya Wizara ya Afya inayoongoza uanzishwaji na usimamiaji katika kutoa huduma bora za Maabara binafsi za afya" amesema Dkt. Katura.

Ameendelea kwa kuwataka, wasimamizi wa huduma za Maabara binafsi nchini kuweka mikakati mbalimbali ya ufuatiliaji wa huduma za Maabara kama inazingatia Sheria na miongozo ya Wizara ili kuleta tija, ufanisi na matokeo chanya katika utoaji huduma kwa wananchi.

Aidha, ameendelea kukumbusha wamiliki wote wa maabara binafsi wasiosajili Maabara zao na wenye madeni nchini kuhakikisha wanasajili Maabara zao na wanalipa madeni yao hadi kufikia tarehe 30 ya mwezi Aprili 2021, na kusisitiza hatua kali zitachukuliwa kwa watakao kiuka agizo hilo.

"Kupitia Mkutano wa PHLB na wamiliki wa Maabara wa Mkoa wa Dar-es-salaam Mwenyekiti wa bodi ya Maabara binafsi alitoa agizo kwa wamiliki wote wa Maabara binafsi nchini kukamilisha ulipaji wa madeni yao hadi kufikia tarehe 30 Aprili 2021, na wasiosajili Maabara zao hivyo hivyo, baada ya hapo hatua kali zitachukuliwa " amesema Dkt. Katura.

Pia Dkt. Katura amewapongeza Waratibu wote kwa kazi wanayoifanya za kusimamia Maabara binafsi katika maeneo yao ili kutoa huduma bora na za viwango kwa wananchi, jambo linalosaidia kupunguza matumizi mabaya ya dawa na muda wa kutafuta huduma za Maabara.

Kwa upande wake Msajili wa Maabara binafsi za afya nchini Bw. Dominic Fwiling'afu amesema kuwa, kikao hicho kina lengo la kupokea taarifa ya utekelezaji wa kazi za usimamizi wa Maabara binafsi kwenye mikoa yao ili kuwatambua mbinu za mafanikio na kutambua changamoto na namna ya kuzitatua changamoto hizo ili kuboresha huduma.

Amesema kuwa, kila Mratibu wa Maabara wa Mkoa aende akaboreshe mahusiano baina yake na Waratibu wenzake wa Halmashauri na Waratibu wengine, huku akisisitiza ushirikiano katika hatua za usajili na katika kujibu kero mbali mbali za wananchi ili kuboresha huduma za Maabara nchini.

Vile vile ametoa wito kwa Waratibu hao kufika katika ngazi zote, ikiwemo ngazi ya kata na mitaa na kuwashirikisha viongozi wa ngazi, kama sehemu ya kushirikiana katika kutoa huduma bora za Maabara kwa wananchi, kwani Maabara nyingihuanzishwa katika ngazi hizo, zikiwemo maabara bubu.

Hata hivyo, Bw Fwiling'afu amesema kuwa, Wizara ya Afya kupitia Maabara binafsi imeanza mikakati ya kuandaa madaraja ya maabara, aina ya vipimo na idadi ya vipimo kulingana na daraja lako, huku akifafanua madaraja hayo ni A,B,C.

Aliendelea kwa kutoa msisitizo kuwa, huduma zinazotolewa kupitia Maabara ni vipimo tu na hairuhusiwi kufanya huduma nyingine za kitabibu kama kutoa dawa, kulaza wagonjwa na kuweka dripu, jambo ambalo ni kinyume na Sheria na miongozo ya uanzishwaji wa huduma za Maabara binafsi nchini.

Nae Mwenyekiti wa Waratibu wa Maabara nchini Bw. Onna Panga ameipongeza Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kuandaa kikao hicho chenye lengo la kuboresha huduma za Maabara nchini kwa kuwakutànisha Waratibu wa Maabara Mkoa na kubadilishana ujuzi juu ya taaluma ya Maabara ikiwemo utatuzi wa changamoto unaowakumba.

Akiwa kama Kiongozi wa Waratibu wa Maabara nchini Bw. Panga amesema kuwa, kama Waratibu wamepokea maagizo na maelekezo kutoka kwa Wizara na kuahidi kuyafanyia kazi kwa muda mfupi ili kuonesha tija na ufanisi katika utoaji huduma za Maabara katika maeneo yao.

Mwisho.



Maabara ya kisasa ya upasuaji wa ubongo (Ango-Suite) katika Taasisi ya Mifupa (MOI) Maabara hii itaiwezesha taasisi kufanya upasuaji wa matatizo ya mishipa ya damu kichwani pasipo kulazimika kufungua fuvu la kichwa.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii Mhe. Stanslaus Nyongo (kushoto) akifafanua jambo kwenye kikao cha kamati hiyo na Wataalam toka Wizara ya Afya.

Mkurugenzi Mtendaji Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete Prof. Mohhamed Janabi (aliyesimama) akiwasilisha taarifa ya taasisi anayoongoza kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii.

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Godwin Mollel (kuhsoto) pamoja na Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Afya Bw. Edward Mbanga wakisoma taarifa za miradi ya maendeleo za taasisi zilizochini ya Wizara ya Afya kwenda Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii.




Na Englibert Kayombo - Dodoma

Kamati ya kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii imeipongeza Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kuendelea kuwekeza na kuboresha upatikanaji wa huduma za tiba za kibingwa nchini na kupunguza gharama za matibabu kwa watanzania waliokuwa wanapata huduma hizo nje ya nchini.


Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Stanslaus Nyongo kwenye kikao cha Kamati hiyo na Wataalam wa Wizara ya Afya na Tasisi zake kilichofanyika kwenye kumbi ya mikutano ya Bunge.


“Nazipongeza Taasisi zote zilizowasilisha taarifa zao, hongera kwa uzalendo wenu wa kuendelea kuokoa maisha ya Watanzania na kuipunguzia Serikali gharama za matibabu nje ya nchi” Amesema Mhe. Nyongo


Mheshimiwa Nyongo amesema kupitia kamati hiyo itaendelea kutoa ushirikiano na Wizara a Taasisi zake kuhakikisha kuwa wananchi wanapata huduma bora za tiba nchini na kupitia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wataendelea kuishauri Serikali kuwekeza zaidi kwenye huduma zia tiba za kibingwa na kuhakikisha huduma zote za tiba zinapatikana hapa nchini na kuvutia zaidi utalii wa tiba (Medical Tourusm) kwa raia wa kigeni wenye uhitaji wa tiba zinazopatikana hapa nchini.


Awali akisoma taarifa ya Taasisi ya Saratani ya Ocean Road Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo Dkt. Julius Mwaiselage amesema kuwa uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali kwa kuimarisha miundombinu ya kutolea huduma za kibingwa katika taasisi hiyo uliohusisha manunuzi ya mashine za kitaalam pamoja na ujenzi wa majengo umewezesha kupunguza rufaa za wagonjwa wa saratani kwenda nje ya nchi kutoka wagonjwa 164 mwaka 2014/15 hadi wagonjwa 5 mwaka 2019/20.


Dkt. Mwaiselage ameendelea kwa kusema kuwa na miundombinu hiyo hapa nchini Serikali imeweza kuokoa fedha kiasi cha shilingi bilioni 10.4 kwa kutopeleka wagonjwa 208 nje ya nchi huku wagonjwa wanaotoka nchi jirani kwa ajili ya tiba imeongezeka kutoka wagonjwa 12 mwaka 2014/15 hadi kufikia wagonjwa 73 mwaka 2019/20 hivyo kuongeza mapato kwa Serikali.


“Kutokana na miundombinu tuliyonayo sasa idadi ya wagonjwa wanaotibiwa kwa siku imengezeka kutoka wagonjwa 170 hadi kufikia wagonjwa 270. Aidha tumeweza kupunguza muda wa kusubiri tiba mionzi kutoka wiki 6 mwaka 2014/15 hadi kufikia ndani ya wiki 2 mwaka 2019/20 muda ambao ndio kiwango kinachokubalika cha kusubiri tiba duniani” amefafanua Dkt. Mwaiselage.


Akiwasilisha taarifa ya Taasisi ya Mifupa (MOI) Dkt. Vivina Wananji amesema kuwa katika kipindi cha miaka minne taasisi hiyo imeweza kufanya upasuaji wa kibingwa kwa wagonjwa 43,200 ambapo kwa gharama za hapa nchini upasauji huo umegharimu kiasi cha Shilingi Bilioni 16.5 na kama wangepelekwa nje ya nchi matibabu yangegharimu kiasi cha Shilingi Biloni 54.9 hivyo kuokoa kiasi cha Shilingi Bilioni 38.4


Dkt. Wananji amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imetoa kiasi cha Shilingi Bilioni 7.9 kwa ajili ya ujenzi wa maabara ya kisasa ya upasuaji wa ubongo (Ango-Suite).


“Maabara hii itaiwezesha taasisi kufanya upasuaji wa matatizo ya mishipa ya damu kichwani pasipo kulazimika kufungua fuvu la kichwa, vilevile mashine hii itakua na uwezo wa kutibu damu iliyoganda kwenye mishipa ya damu miguuni, kwenye moyo, tumbo la uzazi, ini na figo” Amefafanua Dkt. Wananji na kuendelea kusema kuwa matibabu kwa kutumia maabara hiyo ni ya haraka hivyo wagonjwa wengi watapata huduma kwa muda mfupi huku uwepo wa Maabara hii utaifanya Tanzania kuwa moja ya Nchi chache Barani Afrika zinazotoa huduma hiyo.


Kwa upande wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo Prof. Mohhamed Janabi amesema kuwa Taasisi hiyo yenye miaka mitano toka ianzishwe imekuwa ikihudumia wagonjwa kutoka mikoa yote ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambao wamepewa rufaa kutoka Hospitali za mikoa na za wilaya zilizoteuliwa kwa ajili ya kupata huduma ya kiwango cha juu cha tiba ya Moyo, vilevile na wagonjwa wanokuja moja kwa moja kwa matibabu kutoka nje ya nchi.


Prof. Janabi amesema kuwa Serikali kupitia Wizara ya Afya ilitoa kiasi cha Shilingi Bilioni moja kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba vitavyosaidia kuboresha zaidi huduma za kibingwa hapa nchini. 


Amezitaja mashine hizo kuwa ni ‘Intra-Aotic balloon Pump’ inayotumika kutibu wagonjwa wenye matatizo ya kuziba mishipa ya damu, ‘Anaesthesia Machine’ inatumika kutoa dawa ya usingizi kwa ajili ya kulaza wagonjwa wanapoingia kwenye upasuaji wa moyo, ‘ICU ECHO Machine’ ambayo inatumika kwa ajili ya kuangalia uwezo wa moyo kufanya kazi, pamoja na ‘Syringe Pumps’ ambazo hutumika kupeleka vimininika (dawa) kwenye mwili wa binadamu kupitia mishipa ya damu. Vifaa tiba vyote hivi vimenunuliwa kutoka fedha za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.


Mwisho



Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Abel Makubi akisema jambo kwa wazalishaji wa dawa asilia (hawapo pichani) kwenye kikao kilichowakutanisha wazalishaji wa dawa asilia na watendaji kujadili namna bora ya kurahisisha upatikanaji wa dawa asilia kwa jamii.

Dkt. Paul Mhame Mkurugenzi Msaidizi Tiba Asili kutoka Wizara ya Afya akisema jambo kwa wazalishaji wa dawa asilia (hawapo pichani) kwenye kikao kilichowakutanisha wazalishaji wa dawa asilia na watendaji kujadili namna bora ya kurahisisha upatikanaji wa dawa asilia kwa jamii.

Wazalishaji wa dawa asilia na wataalam wa afya wakiwa kwenye kikao cha kujadili namna bora ya kurahisisha upatikanaji wa dawa asilia ndani ya jamii


Na WAMJW - Dodoma

Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto imeweka mkakati wa kusogeza karibu huduma za tiba asili kwa jamii ambazo sasa dawa hizo asilia zinawekewa mikakati ya kupatikana hadi kwenye vituo vya kutolea huduma za afya pamoja na maduka ya kuuza dawa za binadamu.

Hayo yamesewa na Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Abel Makubi mara baada ya kufanya kikao na wazalishaji wa dawa hizo asilia nchini ambao dawa zao zimethibitishwa Usalama na Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali  pamoja na Msajili wa Tiba Asili nchini na kukidhi vigezo vya kutumika kwa binadamu.

“Sisi watendaji tumeona ni muhimu kukutana ili tuweze kuweka mikakati ya kuhakikisha hizi dawa asili zinawafikia wananchini kwa urahisi zaidi”amesema Prof. Makubi.

Amesema kuwa tunasumbuliwa na magonjwa ya kuambukiza na yasiyo ya kuambukiza hivyo ni lazima tutumie silaha (dawa asilia na za kisasa) zote ambazo ni salama zinaweza kusaidia wananchi kwa afya.

“Kuna hizi dawa asili zenye usalama, ambazo zimekuwa zikitumika kutibu magonjwa ya kuambukiza na yasiyoambikiza hivyo ni lazima tuzisogeze karibu kwa wananchi kupitia mawakala, maduka ya madawa ya binadamu nata hospitalini kwa usalama ziweze kuwafikia wananchi” ameeleza Prof. Makubi.

Aidha Prof. Makubi amewataka wasomi na wataalam wa afya kwa ujumla kubadili mtazamo wao juu ya tiba asili kwa kuwa zimekuwa na mchango mkubwa wa kutibu magonjwa mbalimbali ya binadamu na kuwaasa wataalam kutokuwa kikwazo kwa wananchi kutumia tiba asili.

“Kama dawa sisi tumeshaihakiki na tukaikubali kwamba hii dawa ni salama, basi pasiwepo na kinyongo au ugumu wowote wa sisi watumishi wa afya kuruhusu mwananchi kutibiwa kwa dawa hiyo ”Amesisitiza Prof. Makubi.

Katika hatua nyingine Prof. Makubi hakusita kuwaasa wananchi kuendelea kuchukua tahadhari zote za kinga za magonjwa magonjwa yote ikiwemo kufanya mazoezi, kubadili mtindo wa maisha na kula chakula bora. Wananchi siyo lazima wasubiri matamko ya Serikali katika kujikinga na magonjwa; njia nyingi za kujikinga na magonjwa zimeshatolewa na wanazijua; kwa hiyo ni suala la wao kujenga mazoea ya kujikinga kila siku ya Mungu.

Prof Makubi alielezea pia umuhimu wa kufanya tafiti zaidi katika tiba asilia ili ziweze kuhakikia kwa miongozo ya nchi na kimataifa na baadae kuweza hata kuhudumia wananchi wa nchi za jirani. Aidha alisisitiza kuwa Wagunduzi watalindwa na Serikali na kuhakikisha umiliki wa ugunduzi wa dawa hizo haupotei wakati na baada ya utafiti. 

Naye Dkt. Paul Mhame, Mkurugenzi Msaidizi Tiba Asili kutoka Wizara ya Afya amesema kuwa Serikali kupitia Taasisi zake imeweza kuchambua na kuidhinisha dawa za kunywa aina 5 na dawa aina 4 za  mafuta tete  kwa ajili ya kujifukiza ambazo zimekidhidi vigezo kuweza kutumika kwa binadamu. Amezitaja dawa hizo za kunywa kuwa ni NIMRICAF, COVIDOL, BINGWA, PLANET ++ pamoja na COVOTANZA huku zile za mafuta tete zikiwa ni BUPIJI pamoja na UZIMA. 

“Aidha Serikali inaendelea kufanya kazi kwa karibu na wazalishaji wengine ambao wakikidhi vigezo dawa zao zitaongezwa kwenye orodha hii” Amesema Dkt. Mhame na kuwasisitiza wananchi kujitokeza kwenda kununua dawa hizo kwa ajili ya kujikinga na magonjwa ambukizi na yasiyoambukiza.

Akizungumuza kwa niaba ya wazalishaji wa dawa asili Bw. George Buchafwe ambaye ametengeneza dawa ya kujifukiza kwa mafuta tete ya Bupiji ameishukuru Serikali kwa kuona mchango wao na kuwa sehemu ya kuchangia na kuboresha afya za wananchi. 

“Tunaishukuru Serikali kwa kutambua kuwawapo watafiti ambao wanaweza wakaisaidia jamii yetu na ikawezakutoka katika hatua kwenda hatua nyingine kwa kutumia tiba zetu za asili” Amesema Bw. Buchafwe.

Amesema kuwa wao wazalishaji wa dawa za asili wapo tayari kushirikiana na Serikali kuzalisha bidhaa bora ye usalama kwa afya ya binadamu.

Kwa upande wake Dr Otieno kutoka Taasisi ya Tiba Asilia Muhimbili amesisitiza umuhimu wa wananchi kuacha kuchanganya dawa zaidi ya moja kwa wakati mmoja wakati wa kutumia. Amesema ni vema pia wananchi wafuate maelekezo sahihi ya matumizi ya hizi dawa na kuzingatia usalama wake.



MKRdezign

{facebook#YOUR_SOCIAL_PROFILE_URL} {twitter#YOUR_SOCIAL_PROFILE_URL} {google-plus#YOUR_SOCIAL_PROFILE_URL} {youtube#YOUR_SOCIAL_PROFILE_URL} {instagram#YOUR_SOCIAL_PROFILE_URL}

Contact Form

Name

Email *

Message *

Powered by Blogger.
Javascript DisablePlease Enable Javascript To See All Widget