Latest Post

 
Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Gwajima akiongea wakati wa kikao kazi hicho ambapo aliwataka viongozi hao kutekeleza ipasavyo Ilani ya uchaguzi ya mwaka 2020 ya Chama cha Mapinduzi.
 
Baadhi wa watendaji wa wizara ya afya makao makuu wakifuatilia mkutano huo  ambao unajadili maadili na weledi wa wanataaluma kwenye vituo vya vya kutolea huduma nchini.
 
Washiriki wa kikao kazi hicho kwenye ukumbi wa hospitali ya Benjamin Mkapa.
 
 

SIMAMIENI MAADILI NA WELEDI - DKT. GWAJIMA

Na. Catherine Sungura,WAMJW-Dodoma

Vyama, Mabaraza pamoja na bodi za kitaaluma nchini  vimetakiwa kudhibiti maadili na weledi katika utendaji kwa  watumishi wa sekta ya afya nchini ili kuboresha utoaji huduma kwa wananchi.

Hayo yamesemwa leo na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima wakati wa kikao na viongozi hao kwenye ukumbi wa hospitali ya Benjamin Mkapa jijiji Dodoma.

Dkt.Gwajima amesema kuwa vyama, bodi na mabaraza ya kitaaluma ndio wasimamizi wakuu na wadhibiti wa maadili na weledi ambapo wananchi bado wanakutana na changamoto nyingi za maadili na weledi wakati wa upataji  huduma za afya.

"Kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya uchaguzi  kurasa 137 imeandikwa kushirikiana na vyama vya kitaaluma vya kada ya afya katika kusimamia uzingatiaji wa maadili na weledi katika utendaji wa watumishi hilo ndio tunalotekeleza. "Amesisitiza Dkt. Gwajima.

Amesema wanapofanya ziara kwenye mikoa mbalimbali wanakutana na kero zitokanazo na kufifia kwa maadili na weledi wa utendaji, huku akiweka  wazi kuwa, haya yote yanadhibitiwa na vyama, bodi na mabaraza ya kitaaluma.

"Ili tuweze kuhuisha hayo yote, lazima tukae pamoja na kuangalia mifumo yao ya utendaji kazi ukoje hadi unatoa mianya ya baadhi ya wanataaluma kukosa maadili na kuleta malalamiko mengi kutoka kwa wananchi?,Aliuliza Dkt. Gwajima

Aidha, Dkt. Gwajima amesema kutokana na malalamiko hayo inafanya kuonekana kukosa meno ya vyama hivyo vya kitaaluma, hivyo kikao hicho kikubwa ni kuambina ukweli na kuwakumbusha majukumu yao na wafahamu kuna tatizo kwa wanataaluma wao ndio mana hawashtuki na hata wengine kuvunja maadili bila kujali kama kuna mabaraza ya kitaaluma na kubadilika ili kuondoa kero kwa wananchi.

Kwa upande wa kuwa na mwamvuli mmoja wa mabaraza yote ni kwamba itasaidia kuwa na timu moja na matumizi ya fedha ya kuendesha mabaraza yote yatapungua na kuongeza ufanisi na tija ya wataalam wengine ili wakae kwenye maadili.

Naye Naibu Waziri Dkt. Godwin Mollel amewataka viongozi hao kuwajibika ili kuondoa matatizo ambayo ama wao kama mabaraza hawayaoni au yanaonwa na viongozi wa wilaya eneo husika.

Dkt. Mollel aliendelea  kusema kuwa, wataalamu wengi hivi sasa hawafanyi kazi kwa kuzingatia maadili na hivyo kusababisha makosa mengi ya kitaaluma yanafanyika kwenye vituo vya  kutolea huduma na wananchi wengi kupoteza maisha na wengine kupata athari kwenye jamii.

"Tunakuta makosa kwenye taaluma mfano dawa zinaibiwa lakini  wewe mwenye baraza lako na unasimamia maadili hulioni hili hivi hujioni kwamba na wewe unatakiwa kuadhibiwa? Aliuliza Dkt.Mollel.

Hatahivyo amewataka viongozi hao kujitafakari kama wanatosha kwenye mabaraza yao kama wanashindwa wao kugundua matatizo yaliyopo chini kwani wanakuwa wameshindwa kusimamia na kufanya kazi zao vizuri kwa kutoa adhabu kwa wanaofanya makosa na kusababisha matatizo kwa wananchi.

Mwisho.


 



 
Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Abel Makubi akieleza jambo mara baada ya kufanya kikao na Viongozi wakuu wa sekta ya afya kwa njia ya mtandao"ZOOM" kilichowajumuisha  Waganga wakuu wa Mikoa na Wilaya,Wajumbe wa kamati ya usimamizi wa huduma za afya za mikoa(RHMT) na wilaya (CHMT) pamoja na Wakurugenzi wa hospitali za Taifa,Kanda na Maalumu.

 

VIONGOZI SEKTA YA AFYA TATUENI KERO ZA WANANCHI:PROF. MAKUBI  

Na. Catherine Sungura,WAMJW-Dodoma

Wizara ya Afya ipo tayari kupokea kero na malalamiko ya wananchi endapo itaonekana wameshindwa kusikilizwa  ama  kusaidiwa na viongozi wao wa ngazi za chini na wale wa vituo vya kutolea huduma za afya kwenye maeneo yao.

Hayo yameelezwa leo na Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Abel Makubi mara baada ya kufanya kikao na Viongozi wakuu wa sekta ya afya kwa njia ya mtandao"ZOOM" kilichowajumuisha  Waganga wakuu wa Mikoa na Wilaya,Wajumbe wa kamati ya usimamizi wa huduma za afya za mikoa(RHMT) na wilaya (CHMT) pamoja na Wakurugenzi wa hospitali za Taifa,Kanda na Maalumu.

Prof. Makubi amesema kuwa wananchi wana matumaini na Serikali yao hivyo wanayo haki ya kusikilizwa na kutatuliwa kero zao kutoka kwa watendaji kwenye vituo vyote vya  huduma za afya nchini hivyo kamati zote zinapaswa kufanya tathimini za kero zote kwa muda wa wiki nne  na kuzitatua pia  kuwasilisha ripoti Wizarani pamoja na TAMISEMI .

“Tunaanzisha utaratibu ambao sisi viongozi wa sekta ya afya tunaenda kutafuta kero kutoka kwa wananchi na kuzitatua,Hili ni agizo na tumekubaliana wasambae kwenye ngazi zote kuanzia zahanati,vituo vya afya na kwenye hospitali,tunatakiwa kuhakikisha wananchi wapate huduma bora licha ya kuwa tumeboresha huduma kwenye vituo vyetu”.

Aidha, amesema utaratibu huu utaweza kurahisisha kutatua kero za wananchi na kuweza kupunguza kero hizo na zingine sio lazima zimfikie Mhe. Waziri hivyo kama watendaji wanatakiwa kujitafakari wanaweza kutatua vipi changamoto wazipatazo wananchi.

“tumekubalikia suala la kuimarisha suala la uongozi, uwajibikaji na usimamizi  kwani kila mmoja ameona kuna mapungufu kwenye usimamizi wa huduma za afya nchini,hivyo tumekubaliana kila kiongozi kuanzia Taifa hadi vijijini kusimamia sehemu zenye mapungufu kwani wananchi wanahitaji mazuri kutoka kwetu,hatuwezi kuwaridhisha kwa kila kitu lakini tutapunguza matatizo yao.

Upande wa kuimarisha vitengo vya huduma kwa wateja, Mganga Mkuu huyo wa Serikali amesema  kitengo hicho kinatakiwa kuboreshwa na hivyo wanapaswa kuchakata kero zote na kuzifanyia kazi na hivyo kuzibandika kwenye ubao wa matangazo wa vituo vyao pia wanapaswa kuwa hai wakati wote kwakuwa  mwananchi wanataka huduma za afya jinsi wanavyohitaji.

“Viongozi hao pia wanatakiwa kukagua ndani ya  hospitali zao kwenye maeneo ya kutolea dawa na  stoo kuona kama dawa zipo na zinawatosheleza wananchi,kama kuna wizi tuweze kuchukua hatu,waende kwenye wodi na OPD kuwasalimu wagonjwa na kama wana kero waseme ili wazitatue,pia maabara kuweza kuona kama vipimo vinafanyika”.Alisisitiza.
 
Hata hivyo wamekubaliana kuwepo na magroup ya ‘Whatsap’ ambayo watapokea na kushughulikia kero kwenye kila wilaya au mkoa husika ili kila mwananchi awezo kutoa kero zake.

 “Tumeagiza kuwe na namba ambazo zitatangazwa kwa wananchi,pia wawashirikie wananchi kupitia mikutano na kutaja namba zao ili wananchi wajue wanawasilisha vipi malalamiko yao ”.

Aliongeza kuwa wananchi wanapaswa kujenga imani na kuwaamini watendaji wote wa sekta ya afya, na kusema kuwa baada ya Mhe. Waziri kutangaza namba yake ya malalamiko kwa muda wa wiki mbili ameweza kupokea kero elfu tatu kutoka maeneo mbalimbali nchini.

Kikao hicho kwa njia ya mtandao kimehudhuriwa na washiriki wapatao 220 na ajenda kubwa ilikuwa ni jinsi ya kupunguza kero za wananchi zinazousiana na huduma za afya nchini ambazo wanatuma kupitia namba ya malalamiko iliyotangazwa na Waziri wa afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Doroth Gwajima mwishoni mwa mwaka jana ambayo ni 0734124191.

-MWISHO-


 
Mwakilishi wa Katibu Mkuu,Wizara ya Afya na Mkurugenzi Msaidizi wa Tiba Asili/Mbadala Dkt. Paul Mhame akifungua kikao kazi cha usambazaji wa miongozo inayosimamia huduma za tiba kwa Waganga Wakuu wa Mikoa,Wataalamu wa Maabara ngazi ya Mikoa na Wilaya nchini kwenye ukumbi wa Chimwaga jijini Dodoma.
 
Mkuu wa huduma za maabara nchini kutoka Wizara ya Afya Peter Torokaa akiwasilisha miongozo kwa washiriki wa kikao kazi hicho.Jumla ya miongozo 20 imesambazwa.
 
Afisa kutoka Idara ya Huduma za Tiba (Maabara) Bi. Bahati Faki akitoa neno wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha usambazaji wa miongozo inayosimamia huduma za tiba kwa Waganga Wakuu wa Mikoa,Wataalamu wa Maabara ngazi ya Mikoa na Wilaya nchini kwenye ukumbi wa Chimwaga jijini Dodoma. 
 
Washiriki wa kikao kazi hicho ambacho  kimehudhuriwa na watendaji katika ngazi ya Taasisi/Hospitali za Taifa, Mkoa na Halmashauri pamoja na wawakilishi wa Timu za usimamizi huduma ngazi ya Mkoa na Wilaya takriban washiriki 300.
 
Washiriki wa kikao kazi cha usambazaji wa miongozo inayosimamia huduma za tiba wakifuatilia ufunguzi ambapo walisisitizwa kuhakikisha kwamba miongozo hiyo inatumika kwa ufasaha.
 
Kikao kazi cha usambazaji wa miongozo inayosimamia huduma za tiba kwa Waganga Wakuu wa Mikoa,Wataalamu wa Maabara ngazi ya Mikoa na Wilaya nchini kikiendelea kwenye ukumbi wa Chimwaga jijini Dodoma.
 
Picha ya pamoja ikiongozwa na Mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Paul Mhame wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha usambazaji wa miongozo inayosimamia huduma za tiba kwa Waganga Wakuu wa Mikoa,Wataalamu wa Maabara ngazi ya Mikoa na Wilaya nchini kwenye ukumbi wa Chimwaga jijini Dodoma.

 

ONGEZENI KASI KATIKA HUDUMA ZA MAABARA: DKT. MHAME

Na. Catherine Sungura,WAMJW-Dodoma

Wataalam wa Maabara nchini wametakiwa kuongeza kasi katika kuhakikisha huduma za tiba inayotolewa inafuata miongozi ya wizara na kuhakikisha wanabadili fikra na mitazamo ili kuwafanya wateja wao waweze kuvutiwa na huduma wanazozisimamia.

Hayo yamesemwa leo na Mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Afya ambaye ni Mkurugenzi Msaidizi wa Tiba Asili/Mbadala Dkt. Paul Mhame  wakati wa  kikao kazi cha  usambazaji wa miongozo inayosimamia huduma za tiba katika ukumbi wa Chimwaga jijini Dodoma.

Dkt. Mhame amesema kuwa miongozo hiyo itakayowasilishwa kwa siku mbili imesisitiza kuboresha utoaji wa huduma za tiba pia masuala ya usimamizi wa huduma za damu salama pamoja na sheria, kanuni na miongozo ya kusimamia Tiba Asili nchini.

“Hakikisheni masuala haya ambayo ni mtambuka katika utoaji wa huduma mnayaelewa vyema ili muweze kuisaidia jamii, ikumbuke kuwa yapo maelekezo yaliyotolewa na viongozi wa kitaifa hususan suala la tiba asili na tiba mbadala hivyo muhakikishe mnawawezesha waratibu hao pindi inapotokea changamoto katika kusimamia huduma hizi kwenye ngazi mnazosimamia”.Alisisitiza Dkt. Mhame.

Hata hivyo Dkt. Mhame aliwataka washiriki hao kuhakikisha ujumbe utakaotolewa kwenye kikao kazi hiko kitawafikia walengwa ili pindi ukaguzi na usimamizi shirikishi utakapofanyika uwe na tija katika kuboresha huduma za tiba kwenye maeneo waliyotoka na hivyo itasaidia kuboresha huduma za uchunguzi katika hospitali na ngazi mbalimbali za utoaji huduma za tiba nchini.

Naye Mkuu wa huduma za Maabara nchini kutoka Wizara ya Afya Peter Torokaa amewasisitiza vituo vyote vya kutolea huduma za afya nchini kufanyia tathimini ya ufanisi “Calibration” wa  mashine zote kwa kuwatumia wataalam wa maabara na zile zinazotakiwa kufanywa na Shirika la Viwango (TBS) wanafanyia pia kwani ndio wenye mamlaka.


Aidha, Torokaa amewataka Mameneja na Waratibu wa maabara wa Mikoa na Wilaya kuhakiki uwezo wa mashine “Method Verification” kupima na kutoa majibu yaliyo sahihi hivyo kila kipimo kithibitishwe kama kinatoa majibu ya wagonjwa yaliyo sahihi.

“Jambo la tatu tunalosisitiza ni wataalam wetu kupimwa umahiri kwa kuhakikisha mameneja na waratibu wetu wa Mikoa na wilaya  wanasimamia watoa huduma wetu ambao ni wataalamu wa maabara wanafanyiwa umahiri kama wana uwezo wa kutumia hiyo mashine,kifaa na kutoa majibu ikiwemo uwezo wa tafsiri majibu ambayo yanaenda  kwa Daktari kufanya maamuzi kwa mteja.

Aliongeza kuwa kila kipimo lazima kifanyike kidhibiti ubora kabla maabara haijatoa majibu kwenda kwa daktari kuhakikisha inadhibiti majibu hayo ndani ya maabara kwa kila kipimo pamoja na kuhakikisha maabara inashiriki sampuli zingine  ndani na nje ya nchi ili kuweza kujipima kama wanaweza kutoa majibu yaliyo sawa.

Naye Meneja wa Maabara wa Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Tanga-Bombo  Sinde Mtobu amesema maabara yao imekuwa miongozi wa uboreshaji wa huduma nchini na kuwa katika ngazi ya  nyota nne hivyo wanasubiri kupata ithibati ya kimataifa IS0-15-18-9 kwenye huduma za ubora kwa ujumla hivyo wapo miongoni mwa maabara 27 nchini.

Ametaja  moja ya eneo ambalo wamefanya vizuri kwenye maabara ni  kuwawezesha wataalam wa maabara kwenye umahiri kwa kusimamia miongozo yote pamoja na eneo la uhakiki ubora  wa huduma zao kabla ya kwenda kwa daktari.


MWISHO



 Msajili wa Baraza la Famasi Bi. Elizabeth Shekalaghe akisisitiza jambo wakati akiongea na afisa habari wa Wizara ya Afya,ofisini kwake jijini Dodoma.

 

 WAFAMASI WAKUMBUSHWA KUHUISHA LESENI ZAO KABLA MWAKA KUISHA

Na. Catherine Sungura,WAMJW-Dodoma

Wafamasia, fundi dawa sanifu na wasaidizi nchini wamekumbushwa kuhuisha leseni zao kabla ya tarehe 31 Disemba mwaka huu ili waweze kuendelea kufanya kazi za kitaaluma kwa mwaka unaokuja.

Wito huo umetolewa leo na Msajili wa Baraza la Famasi Bi. Elizabeth Shekalaghe wakati akiongea na afisa habari wa Wizara ya Afya,ofisini kwake jijini Dodoma.

Bi. Elizabeth amesema kuwa kwa mujibu wa kifungu Namba 22 cha Sheria ya Famasi, Sura 311 kinawataka wafamasia kuweza kuhuisha majina yao kwenye rejista kwa utaratibu maalamu.

"Pamoja na baraza la famasi kuwasajili wanataaluma kwa mujibu wa kifungu cha sheria ya famasi nchini,kifungu kinatutaka kabla ya tarehe 31 Desemba ya kila mwaka kuhuisha majina ili kuweza kufanya kazi  za kitaalam kwa mwaka unaokuja".Alisisitiza Msajili

Kwa upande wa uuzaji wa dawa Msajili wa Baraza hilo Bi.Shekalaghe amesema  tatizo la uuzaji wa dawa kiholela limekuwa ni tatizo sugu hapa nchini na hivyo mwaka huu Waziri wa Afya ameidhinisha kanuni za udhibiti na usimamizi wa uuzaji wa dawa za cheti na hivyo amewataka wanataaluma wa famasi kuhakikisha wanazisoma na kuzielewa kanuni hizo.

"Kama wafamasia na wataalam tukumbuke tuna watu tunawasimamia na kuhakikisha dawa tunazitoa kwa kuzingatia miongozo iliyopo na Baraza halitosita kumchukulia hatua yeyote atakayeenda kinyume na kanuni hizo".Aliongeza Bi. Shekalaghe.

Mbali na hayo Bi. Shekalaghe amewataka wananchi  kutoa taarifa kwenye Baraza hilo pale wasiporidhika na huduma zitolewazo katika Famasi na maduka ya dawa muhimu kwa kupiga 0736 222 504 au namba bila malipo 0800110015 ili waweze kutatua changamoto wanazozipata wakati wanapatiwa huduma hizo. 


-MWISHO-



Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima akisisitiza jambo wakati wa kikao kazi cha kujadili hali ya utoaji huduma za afya nchini ambacho kimewakutanisha Wakurugenzi wa Wizara pamoja na Taasisi zake kilichofanyika kwenye ukumbi wa hospitali ya Benjamin Mkapa jijini Dodoma.

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto Dkt. Godwin  Mollel akieleza jambo wakati wa kikao kazi cha kujadili hali ya utoaji huduma za afya nchini ambacho kimewakutanisha Wakurugenzi wa Wizara pamoja na Taasisi zake kilichofanyika kwenye ukumbi wa hospitali ya Benjamin Mkapa jijini Dodoma.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima akisisitiza jambo wakati wa kikao kazi cha kujadili hali ya utoaji huduma za afya nchini Kulia kwake ni Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel na kushoto kwake ni Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Bw. Edward Mbanga.


Baadhi  ya Wakurugenzi kutoka Taasisi za Wizara  ya Afya wakifuatilia kwa makini neno kutoka kwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima (hayupo kwenye picha) wakati wa kikao kazi cha kujadili maendeleo ya Sekta ya Afya, kilichofanyika kwenye ukumbi wa hospitali ya Benjamin Mkapa jijini Dodoma.

Wakurugenzi wa Wizara ya Afya pamoja na Wakurugenzi wa Taasisi zake wakiwa katika kikao kazi cha kujadili hali ya utoaji huduma za afya nchini kilichoongozwa na Waziri  wa Afya Dkt. Dorothy Gwajima, kikao kimefanyika katika ukumbi wa hospitali ya Benjamin Mkapa jijini Dodoma.



SERIKALI KUJA NA MFUMO WA TEHAMA WA UFUATILIAJI DAWA

Na. Catherine Sungura,WAMJW-Dodoma.

Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii,Jinsia, Wazee na Watoto inatarajia kuanzisha mfumo wa Tehama kufuatilia mnyororo mzima wa utoaji wa dawa kwenye vituo vya kutolea huduma za afya vya umma vyote nchini.

Hayo yamesemwa leo na Dkt. Dorothy Gwajima, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto wakati wa kikao kazi cha kujadili hali ya utoaji huduma za afya nchini ambacho kimewakutanisha Wakurugenzi wa Wizara pamoja na Taasisi zake kilichofanyika kwenye ukumbi wa hospitali ya Benjamin Mkapa jijini Dodoma.

Dkt. Gwajima amesema kuwa, mfumo huo utasaidia kufuatilia utoaji wa dawa unaofanywa na watoa huduma za afya kwenye vituo vya umma , kwani  Serikali haitaji  upotevu  wa dawa kwenye vituo vyake.

"Tunataka mfumo huu uunganishe vituo vyote pamoja na hospitali zote hadi za Taifa kwani huu ni ulimwengu wa Tehama,hivyo kama kiongozi anatakiwa kuona kila kitu pale alipo ili kuweza kurahisisha kutatua matatizo ya wananchi wetu na hivyo tutadhibiti upotevu wa dawa kwani imekua ni changamoto kubwa na sio kwamba dawa hamna".Alisema Dkt. Gwajima.

Hata hivyo, Dkt. Gwajima aliwakumbusha watoa huduma kutoa dawa kwa kufuata muongozo wa utoaji wa dawa kwa kuandika jina la dawa na sio jina la kampuni kwani kwa kufanya hivyo inasababisha kukosekana kwa dawa ilhali dawa zipo kwenye stoo.

Kwa upande mwingine, Dkt. Gwajima,  ameagiza kufufuliwa na kukanza vikao mara moja  kwa kamati za dawa kuanzia ngazi ya Taifa hadi Zahanati,  ili kuweza kujadili dawa zote zinazotumika kwenye vituo vyao jambo ambalo litasaidia kugundua upotevu wa dawa  kwenye vituo vya umma.

Naye, Naibu Waziri Dkt. Godwin Mollel amesema  kikao kazi hicho kitasaidia kujua changamoto na kuzijadili kwa pamoja  ili kuweza kuwasaidia wananchi  kupata matibabu bora na huduma zingine  kwenye taasisi zilizopo chini ya wizara hiyo kwa urahisi.

Amesema kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita  uwajibikaji na uadilifu umefanyika na hivyo nchi kufanya mapinduzi makubwa kwa kutumia mapato ya ndani, Serikali inayo uwezo wa kununua dawa,vifaa na vifaa tiba  na kutoa matibabu kwa wananchi kwa gharama nafuu na hivyo itawaondolea wananchi mzigo mkubwa wa matibabu nchini.

Dkt. Mollel amewataka watumishi kufanya kazi kwa uaminifu na uadilifu ili kuondoa matatizo yalipo, kwani asilimia 75 ya matatizo hayo  yanaweza kutatuliwa na wenyewe bila kutegemea mtu mwingine, hivyo kuwataka kuongeza kasi ya utendaji kazi na kutumia mapato vizuri ili kuweza kuboresha huduma za afya nchini na kuiongezea mapato Serikali na kusiwepo upungufu wa dawa kwa kuweza vipaumbele maeneo muhimu.
-MWISHO-


 
Mkurugenzi wa huduma za kinga kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Leonard Subi akitoa maelekezo  kwa Maafisa Afya mazingira (hawapo kwenye picha) katika kilele cha wiki ya usafi wa mazingira kitaifa na mkutano wa maafisa afya wa mikoa na halmashauri iliyofanyika jijini Dodoma.
 
Mkurugenzi msaidizi wa Afya mazingira Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Khalid Massa akimkaribisha Mkurugenzi wa huduma za kinga Wizara ya Afya Dkt. Leonard Subi (hayupo kwenye picha) wakati wa kilele cha wiki ya usafi wa mazingira kitaifa na mkutano wa maafisa afya wa mikoa na halmashauri iliyofanyika jijini Dodoma.
 
 
Maafisa Afya  mazingira kutoka ngazi ya Mikoa na Halmashauri wakifuatilia neno kutoka kwa Mgeni rasmi ambae ni Mkurugenzi wa Huduma za Kinga Wizara ya Afya Dkt Leonard Subi wakati wa kilele cha wiki ya usafi wa mazingira kitaifa iliyofanyika jijini Dodoma.
Picha ya pamoja ikiongozwa  na Mgeni rasmi ambae ni Mkurugenzi wa huduma za Kinga Wizara ya Afya Dkt. Leonard Subi pamoja na washindi wa tuzo za uandishi wa habari za usafi  wa mazingira, Jijini Dodoma.


SERIKALI KUBORESHA MAENEO YA KUTUPA TAKA:DKT. SUBI

Na.Catherine Sungura,WAMJW-Dodoma

Serikali ya awamu ya tano ina nia ya dhati ya kuboresha maeneo ya kutupia taka hususani madampo yaliyopo kwenye miji ili yawe ya kisasa.

Hayo yamesemwa leo na Dkt. Leonard Subi  Mkurugenzi wa huduma za kinga kutoka Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto kwenye kilele cha wiki ya usafi wa mazingira kitaifa na mkutano wa maafisa afya wa mikoa na halmashauri iliyofanyika jijini Dodoma.

Dkt.Subi amesema kuwa,uchafuzi wa mazingira utokanao na taka ngumu umeendelea kuwa changamoto katika maeneo ya mijini.

"Ili kukabiliana na tatizo hili,Serikali imepanga kuongeza nguvu kwenye mamlaka za serikali za mitaa ili kuboresga miundombinu katika mitaa iliyopo nchini hasa katika suala la usimamizi wa taka ngumu na majitaka".

Aidha,Dkt. Subi amesema serikali imeandaa mwongozo wa uwekezaji katika taka ngumu ili kuhamasisha uwekezaji na kuongeza jitihada za kuboresha usimamizi wa taka hapa nchini.

Hata hivyo alizitaka halmashauri zipitie sheria ndogo za halmashauri ili kutekeleza vema,Sheria ya Afya ya Jamii ya mwaka 2009 hususani katika maeneo ya utiririshaji maji taka hasa katika maeneo ya mijini na kudhibiti tabia ya kujisaidia porini wakati wa kusafiri maarufu kama ' kuchimba dawa’ ambayo bado imeendelea kuwepo.

Dkt.Subi aliwapongeza maafisa afya hao katika maeneo ya ujenzi wa vyoo bora,unawaji wa mikono ,huduma za afya mipakani,udhibiti wa kipindupindu,Corona,mlipuko wa Dengue pamoja na udhibiti wa taka zitokanazo na huduma za afya na mengine mengi.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Maafisa Afya Tanzania (CHAMATA) Twaha Mubarak ameishukuru Wizara ya afya kwa kufanya afya mazingira ni kipaumbele katika kuondoa magonjwa,hivyo wataalam wanajivunia na kuweza kupunguza ugonjwa wa Malaria ili kuweza kufanikiwa kutimiza lengo la kutokomeza Malaria ifikapo mwaka 2030.

 



MKRdezign

{facebook#YOUR_SOCIAL_PROFILE_URL} {twitter#YOUR_SOCIAL_PROFILE_URL} {google-plus#YOUR_SOCIAL_PROFILE_URL} {youtube#YOUR_SOCIAL_PROFILE_URL} {instagram#YOUR_SOCIAL_PROFILE_URL}

Contact Form

Name

Email *

Message *

Powered by Blogger.
Javascript DisablePlease Enable Javascript To See All Widget