Latest Post

 
Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Prof. Mabula Mchembe akifungua Mkutano wa Maafisa Afya mazingira uliofanyika Jijini Dodoma.
 
Kaimu Mganga Mkuu wa Serikali, ambae pia ni Mkurugenzi wa huduma za Kinga Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Leonard Subi akiwasilisha maelekezo ya Mganga Mkuu wa Serikali kwa Maafisa Afya mazingira katika ufunguzi  wa Mkutano wa tathmini wa Maafisa Afya mazingira uliofanyika Jijini Dodoma.
 
 
Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe TAMISEMI Dkt. Paul Chawote akitoa neno kwa Maafisa Afya mazingira (hawapo  kwenye picha) walio hudhuria Mkutano wao wa tathmini, uliofanyika Jijini Dodoma.

 
Mwenyekiti wa Maafisa afya mazingira nchini Bw. Evans Simkoko akitoa salam za Maafisa Afya mazingira kwa Mgeni rasmi ambae ni Katibu Mkuu Wizara ya Afya (hayupo kwenye picha) wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa tathmini wa Afya mazingira uliofanyika Jijini Dodoma.
 
 
Maafisa Afya kutoka maeneo ya mipaka wakifuatilia kwa makini neno kutoka kwa Katibu Mkuu Wizara ya Afya (hayupo kwenye picha) wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa tathmini wa Afya mazingira uliofanyika Jijini Dodoma.
 
Maafisa  Afya mazingira wakifuatilia kwa makini neno kutoka kwa Katibu Mkuu Wizara ya Afya (hayupo kwenye picha) wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa tathmini wa Afya mazingira uliofanyika Jijini Dodoma.


TIMIZENI WAJIBU WENU KWA WELEDI NA MAADILI.

Na Rayson Mwaisemba, WAMJW- DOM.

KATIBU Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Idara kuu ya Afya Prof. Mabula Mchembe amewataka Maafisa Afya ngazi zote kufanya kazi zao kwa weledi na kufuata maadili wakati watimizapo majukumu yao katika jamii.

Prof. Mchembe ameyasema hayo, wakati akifungua Mkutano wa Maafisa Afya mazingira wenye kauli mbiu ya "Zingatia mahitaji ya Jinsia kwa usafi wa mazingira endelevu " uliofanyika Jijini Dodoma.

"Tusimamie maadili sana, usitende kitu kwa kufikiria kwamba unamfanyia fulani, natambua changamoto zipo katika baadhi ya sehemu, lakini tunahitaji kutimiza wajibu wetu kwa maadili na uwaminifu wa hali ya juu" alisema Prof. Mchembe.

Pia, Prof. Mchembe amewataka Maafisa Afya mazingira kusimamia usafi katika maeneo ya huduma za vyoo katika jamii, hususan katika ofisi na vituo vya daladala ambavyo huudumia Jamii kwa kiasi kikubwa ili kuikinga Jamii dhidi ya magonjwa ya milipuko.

Aidha, Prof. Mchembe amewaagiza Maafisa Afya mazingira nchini kusimamia usafi na ubora wa vyakula katika maeneo yote yanayotoa huduma za vyakula, yakiwemo maeneo ya migahawa na hoteli ili kuikinga jamii na magonjwa ya tumbo na kuhara.

Mbali na hayo Prof. Mchembe ametoa wito kwa Maafisa afya mazingira kujiepusha na vitendo vya Rushwa wakati wa wakitimiza majukumu yao na kuhakikisha usafi wa mazingira unaendelea kufuatwa katika ngazi zote za Jamii.

"Tuachane na Rushwa, inawezekana baadhi ya sehemu unafika pale, unapewa 10,000 au unapewa bia mbili au tatu unaondoka zako, kitu ambacho hakina maana, sasa kama wewe ni Mtaalamu wa Afya simama kwenye maadili yako" alisema Prof. Mchembe.

Hata hivyo, Prof. Mchembe amewaagiza Maafisa afya mazingira nchini, kusimamia udhibiti wa takataka zinazotokana na utoaji wa huduma za afya ili kuendelea kuikinga jamii dhidi ya maambukizi yatokanayo na taka hizo.

Naye Kaimu Mganga Mkuu wa Serikali, ambae pia ni Mkurugenzi wa huduma za Kinga Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Leonard Subi amewaagiza Waganga wakuu wa mikoa  kutoa elimu mara kwa mara kwa watendaji wao juu ya maadili badala ya kusubiri kuchukua hatua baada ya kosa kujitokeza.

"Kutoa elimu mara kwa mara kuhusu maadili, badala ya kusubiri kuchukua hatua kwa Maafisa Afya au wana taaluma wenu, wanapokiuka au kufanya makosa mbali mbali " alisema Kaimu Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Subi.

Aliendelea kusema kuwa, baadhi ya maeneo hususan mijini bado kuna hali ya usafi wa mazingira usioridhisha, na kuelekeza kuanza kampeni ya usafi wa mazingira ya muda wa miezi miwili, huku akiwataka kuanza oparesheni hiyo kwa kuzingatia Sheria na kanuni za afya ya mwaka 2009.

Hata hivyo, Kaimu Mganga Mkuu wa Serikali amewaagiza Maafisa Afya mazingira, kukagua suala la usafi wa mazingira kwenye shule, mabweni, maofisi na maeneo yote yenye mikusanyiko ili kuhakikisha usafi wa mazingira unapewa mkazo ili kuikinga jamii dhidi ya maambukizi ya magonjwa ya mlipuko.

Wakati huo huo Mwenyekiti wa Maafisa afya mazingira nchini Bw. Evans Simkoko ameiomba Serikali kuipa kipaumbele kada ya Maafisa Afya mazingira kwenye ajira mpya, ili kuongeza ufanisi katika utoaji huduma kwa wananchi, kisha kuikinga Jamii dhidi ya maambukizi ya ugonjwa ya milipuko.

Mwisho.


Prof. Mabula Mchembe, 
Katibu Mkuu 
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto

Dkt. Leonard Subi
Mkurugenzi wa Huduma za Kinga
Wizara ya Afya


 Na. Catherine Sungura,WAMJW-Dodoma

Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendheleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Prof. Mabula Mchembe amewapongeza viongozi na watumishi wa huduma za chanjo ngazi zote nchini kwa  utendaji bora wa utoaji wa chanjo kwa bidii na kuhakikisha kuwa malengo yaliyowekwa kitaifa na kimataifa yanafikiwa.

Pongezi hizo zimetolewa leo wakati akifungua mkutano wa mwaka wa tathimini wa huduma za chanjo Tanzania unaofanyika kwenye ukumbi wa Mt. Gasper jijini Dodoma.

"Niwapongeze kwa jitihada zenu na kuifanya nchi kufanikiwa katika utoaji wa huduma za chanjo kwa kuvuka kiwango cha asilimia 90 kilichowekwa kimataifa, hivyo nawataka mkubaliane na kupanga mbinu na mikakati ya kudumisha na kuboresha zaidi viwango vya chanjo nchini".

Hata hivyo katibu Mkuu huyo alisema licha cha kufanikiwa huko Serikali kupitia Wizara yake itaendelea kudumisha  kiwango cha chanjo nchini na ana uhakika takwimu za mwaka 2020  zitakapotolewa na Shirika la Afya Duniani(WHO)  itafikia asilimia 98 au zaidi.

Licha ya pongezi hizo Prof. Mchembe  amewaagiza viongozi wa afya ngazi za Mikoa na wilaya  kuhakikisha kuwa huduma za chanjo zinapewa kipaumbele  ili usitokee tena mkoa utakaoshindwa kudumisha kiwango kilichofikiwa kwani ili watoto waendelee kuwa na afya njema hakuna budi kuwapa chanjo bora za kuwakinga dhidi ya maradhi.

"Nchi yetu imekuwa na utekelezaji wa mkakati wa Fikia kila Wilaya,Fikia kila mtoto apate chanjo,nawasisitiza waratibu wa huduma za chanjo kuhakikisha kuwa mikoa inayofanya vibaya inatumia mkakati huu ili  kuhakikisha kuwa watoto na walengwa wote wanafikiwa katika kupata haki yao ya msingi ya chanjo".

Aidha, Prof. Mchembe aliwashukuru wadau wote wa maendeleo kwa michango yao mbalimbali  katika kuhakikisha kwamba watoto  wanapatiwa chanjo bora  ambayo inaleta kinga dhidi ya maradhi ambayo yanaweza kusababisha ulemevu na vifo kwa watoto.

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe kutoka Ofisi ya Rais-TAMISEMI  Dkt. Ntuli kapologwe amewapongeza Waganga Wakuu wa Mikoa pamoja na waratibu wa huduma za chanjo nchini kwa kuwa kinara wa utoaji wa chanjo na kuweza kuwafikia walengwa wote nchini na kuongoze kuwa TAMISEMI inaipa uzito mkubwa suala la chanjo kwani kinga ya mtoto inaanza na chanjo.

Kwa upande wake  Mwakilishi wa Mganga Mkuu wa Serikali ambaye pia ni  Mkurugenzi wa Idara ya kinga Kutoka Wizara ya afya, Dkt. leonard Subi amesisitiza kuwa wizara ya afya inasimamia ubora na usalama wa huduma wanazozitoa hasa upande wa chanjo ambao mara kadhaa umekua na mapokeo tofauti,hivyo amesisitiza kuwa wizara ipo makini zaidi na afya za wananchi

Wakati huo huo Mwakilishi wa wadau wa maendeleo ambaye anatoka WHO Nassoro Mohamed  ameipongeza Wizara ya afya pamoja na viongozi wa mikoa kwa kuhakikisha watoto wote nchini wanafikiwa  licha ya changamoto za hapa na pale hivyo kama wadau wanashiriki ili kuhakikisha Serikali inafikia malengo waliyojiwekea katika kutoa huduma za chanjo.

-MWISHO-



 
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima akifurahia jambo na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Godwin Mollel baada ya kuwasiri katika ofisi za Wizara ya Afya Jijini Dodoma.
 
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima akisaini kitabu pindi alipowasiri katika ofisi za Wizara ya Afya Jijini Dodoma.
 
 
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Godwin  Mollel akisaini kitabu baada ya kuwasiri katika ofisi za Wizara ya Afya Jijini Dodoma.
 
Katibu  Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Prof. Mabula  Mchembe akisisitiza  jambo mbele ya Watumishi wa Afya wakati  wa mapokezi ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na Naibu Waziri wake katika ofisi za Wizara ya Afya Mtumba Jijini Dodoma.

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Godwin  Mollel akisalimiana na Watumishi wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto pindi alipowasiri katika ofisi za Wizara ya Afya Mtumba Jijini Dodoma.

 

Watumishi wa Wizara ya Afya na Wakurugenzi wake, wakifuatilia kwa makini maelekezo kutoka kwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto katika ofisi za Wizara ya Afya Mtumba Jijini Dodoma.

Picha ya pamoja ikiongozwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima pamoja na Naibu Waziri wake Dkt. Godwin Mollel, wakiwa na Katibu Mkuu Idara ya Afya, Prof. Mabula Mchembe (wanne kutoka kushoto) na Katibu Mkuu Idara ya Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu (wakwanza kushoto).

Picha ya pamoja ikiongozwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima pamoja na Naibu Waziri wake Dkt. Godwin Mollel, wakiwa na Katibu Mkuu Idara ya Afya, Prof. Mabula Mchembe (wanne kutoka kushoto) na Katibu Mkuu Idara ya Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu (wakwanza kushoto), pamoja na Watumishi na Wakurugenzi kutoka Idara Kuu ya Afya.


 

DKT. GWAJIMA AWATAKA VIONGOZI WA WIZARA YA AFYA KUSHIRIKIANA ILI KUONGEZA UFANISI KAZINI

Na WAJMW-Dodoma

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima amewataka Wakurugenzi na watumishi wa Wizara ya Afya kushirikiana ili kuweza kufikia lengo la kuboresha huduma za afya nchini.

Dkt. Dorothy amesema hayo leo wakati akiongea na Wakurugenzi pamoja na viongozi mbalimbali waliompokea mara baada ya kuapishwa na Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli kuwa Waziri wa Wizara hiyo mapema katika hafla iliyofanyika Ikulu-Chamwino, Jijini Dodoma.

Dkt. Gwajima amesema ili sekta ya afya iweze kusonga mbele na kuwafikia wananchi katika kiwango cha hali ya juu inategemea na ushirikiano utakaokuwepo baina ya viongozi wa Wizara pamoja na watumishi mbalimbali wa sekta ya afya.

“Wapeni ushirikiano makatibu wakuu, mambo mengi yanafanywa na wataalam kwa kushirikiana na makatibu wakuu, tukikubaliana kufanya jambo basi wote tufunge mikanda kuhakikisha tukamalisha kwa wakati lengo likiwa kutimiza dhamira ya Mhe. Rais ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya nchini”. Amesema Dkt. Gwajima.

Aidha, Waziri Gwajima amewataka viongozi wa idara mbalimbali wanapotembelea maeneo mbalimbali ya Sekta kuja na ripoti ya ziara zao na kukabidhi kwa Katibu Mkuu ili ziweze kufanyiwa kazi na kutoa miongozo halikadhalika amewataka makatibu wakuu kutofungia ripoti hizo makabatini bali wazifanyie kazi na kutatua changamoto zinazozikabili sekta ya afya.

“Nawataka Viongozi wa Wizara mnapoenda 'Supervision' mrudi na ripoti na pia nawaomba Makatibu Wakuu msizipuuze ripoti mnazoletewa ili tuone zinaleta faida gani kwenye ofisi zetu na pia katika kuboresha huduma za afya nchini”. Ameongeza Dkt. Gwajima.

Waziri huyo amesema kwa kufanya hivyo itaongeza ufanisi kwa kila kiongozi atakayeenda ili kujua aanzie wapi na siyo kila mmoja kwenda na jambo lake huku akiendelea kusisitiza viongozi hao kushirikiana ili kutatua kero na changamoto zilizopo.

Pamoja na hayo Waziri Dorothy amezitaka Taasisi, Hospitali na vituo vya afya kutoa taarifa za mapato na matumizi na ameagiza kutengenezwa mfumo utakaosaidia kupata taarifa hizo ili ziweze kusaidia kutoa muelekeo wa uboreshaji wa huduma za afya.

Pia ametaka utengenezwe muongozo wa huduma kwa wateja ili utolewe kwa watumishi wa sekta ya afya ili wabadilike na kuwathamini wagonjwa wanaofika katika maeneo ya kazi ili kupata huduma.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Prof. Mabula Mchembe amewapongeza na kuwashukuru Waziri Dorothy pamoja na Naibu Waziri Dkt. Godwin Mollel kwa kuchaguliwa kuiongoza Wizara hiyo na kuahidi kutoa ushirikiano.

MWISHO



Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Abel Makubi aliyesisimama akisema jambo kwenye kikao na watumishi wa afya katika Hospitali ya Wilaya ya Kwimba

Watumishi wa afya katika Hospitali ya Wilaya ya Kwimba wakiwa kwenye kikao na Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Abel Makubi (hayupo pichani)

NA Englibert Kayombo WAMJW - Mwanza

Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Abel Makubi ametoa muda wa siku 14 kwa baraza la madaktari pamoja na baraza la wauguzi kwenda Mkoa wa Mwanza kuzungumza na watumishi wa kada wanazosimamia ili kurekebisha na kuwajengea uelewa zaidi wa maadili ya taaluma zao.

Prof. Makubi ametoa agizo hilo akiwa Wilayani Kwimba alipokuwa ziara ya kikazi kukagua hali ya utoaji wa huduma na kuzungumza na watumishi wa kada ya afya. 

“Mabaraza mengi yamekuwa yanabaki huko makao makuu kuhukumu watu, wamejiondoa kabisa kwenye kazi ya kuwajenga watumishi, badala ya kupita huku na kuwaelekeza watumishi, wao wanasubiri kupokea malalamiko” amesema Prof. Makubi

Amesema ni lazima mabaraza yahakikishe watumishi hawafanyi makosa kwa kuwaweka katika maadili mema bila kufanya hivyo tutakuwa na watumishi wasio na sifa.

Prof. Makubi amesisitiza kuwa mabaraza yote 10 yanatakiwa kutelekeza majukumu yao ipasavyo na yote wajiwekee utaratibu wa kuzunguka na kuzungumza na watumishi kuanzia ngazi ya Mikoa hadi Wilayani

Mwisho.



MKRdezign

{facebook#YOUR_SOCIAL_PROFILE_URL} {twitter#YOUR_SOCIAL_PROFILE_URL} {google-plus#YOUR_SOCIAL_PROFILE_URL} {youtube#YOUR_SOCIAL_PROFILE_URL} {instagram#YOUR_SOCIAL_PROFILE_URL}

Contact Form

Name

Email *

Message *

Powered by Blogger.
Javascript DisablePlease Enable Javascript To See All Widget