Latest Post

Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Abel Makubi


Na.WAMJW-Dodoma

Mganga Mkuu wa Serikali Prof.Abel Makubi amewataka Waganga Wakuu wa Mikoa, Wilaya, Wakurugenzi wa taasisi, vyuo vya afya, na waganga wafawidhi kuhakikisha wanawafuatilia kwa karibu wanataaluma wa afya walio katika mafunzo kwa vitendo , yaani watarajali (interns) ili waweze kupata umahiri(competences), utalaamu(skills) na maadili yanayotegemewa. 

Prof. Makubi ameyabainisha hayo wakati akiongea na wasajili wa Mabaraza ya kitaaluma yaliyopo chini ya wizara afya katika ukumbi wa wizara jiji hapa.

Prof. Makubi alisema Serikali imeenza kupata changamoto za baadhi ya Hospitali kushindwa kuwapa mafunzo stahili  wataraji hao na kujikuta wanamaliza mafunzo yao bila umahiri unaotegemewa katika kutoa huduma kwa wananachi.

"Serikali imeanza kuchunguza hizo hospitali na kama hazitasimamia vyema hawa wanataaluma walio mafunzoni, tutazifutia kibali cha kuwapokea"Alisisitiza 

Aidha, Prof. Makubi aliwataka wanafunzi walio kwenye mafunzo kwa vitendo kujituma katika mafunzo yao, kuonyesha nia ya kujifunza na kuweka bidii katika mafunzo yao ya vitendo mahali walipo. 

"Hawa wanataaluma wanapaswa kuonyesha tabia njema wakati wa mafunzo, kuwa watiifu, kulinda viapo vyao kuzingatia maadili ya taaluma zao na kujiheshimu katika lugha zao na hata mavazi wanayovaa mbele ya wateja wao ambao wengi ni wagonjwa na ndugu zao"Aliongeza. 

Hata hivyo Prof. Makubi ameyaagiza mabaraza hayo kuhakikisha utaratibu wa watarajali 'interns' wote kufanya mitihani baada ya mafuzo, uharakishwe ndani ya   mwaka huu ili serikali iweze kupima umahiri wa wanataaluma wote wanaomaliza mafunzo kwa vitendo.

Prof. Makubi aliipongeza Baraza la  Famasi  kwa kuratibu mitihani kwa wafamasia wataraji  na kulitaka  Baraza la Madaktari nalo likamilishe utaratibu wa mitihani kwa madaktari watarajali wote ili kulinda hadhi ya taaluma ya tiba na viwango vya kutoa huduma kwa wananchi.





Mganga Mkuu wa Serikali wa Serikali Prof. Abel Makubi

Na. WAMJW-Dodoma

Wanataaluma wote wa sekta ya afya nchini wametakiwa wawe wamejisajili, na kuhuisha leseni kwenye mabaraza yao ya kitaalam ndani ya miezi sita kuanzia sasa. Aidha kwa wale ambao wamejiendeleza zaidi kitalaamu wanatakiwa kuwasilisha(update) vyeti vyao vya viwango katika mabaraza ili kutambulika kisheria na kitaaluma. 

Rai hiyo imetolewa leo na Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Abel Makubi wakati akiongea na wasajili wa mabaraza mbalimbali ya kitaalam ya Wizara ya Afya pamoja na wasajili wa bodi zilizo chini ya wizara hiyo.

“Kila mwanataaluma aliyemaliza mafunzo yake ni vizuri awe amesajiliwa katika mabaraza yao, agizo hili ni kwa wanataaluma wote katika sekta ya afya ili muweze kutambulika, na uzuri hivi sasa kuna tovuti hivyo mnaweza kupata kujisali , kulipia na baadae kutumiwa  vyeti vyenu bila kuchelewa.  Kwa mantiki hiyo nawapa miezi sita wawe wamesajiliwa”. Alisisitiza

Pia wanatataaluma wanaojiendelea kwa ngazi mbalimbali ya taalauma ya afya kama uzamili na uzamivu 'PhD’ wanatakiwa kusajili hivi viwango katika mabaraza yao ili watambulike. 

Prof. Makubi amesema utaratibu huo umewekwa na Serikali kupitia mabaraza hayo hivyo kila mwana taaluma anatakiwa kujisajili au kuhuisha leseni ambazo zimeisha muda ili waendelee kutambulika na kufanya kazi zao.

Aidha,Prof. Makubi ameongeza kuwa wizara kupitia mabaraza hayo imeweka miundombinu ya mafunzo endelevu ya kitaaluma kwa kila taaluma kwa kufanya mitihani kwa ngazi zote."Lakini mtu aliyefanya mtihani nje ya utaratibu huu basi anatakiwa kuleta  ili kufanya usajili ili kupata alama na uwekwe kwenye kiwango stahili na ndio utaonekana bado upo kwenye kiwango cha uelewa kwenye taaluma yako na kuwatumikia wananchi”.

Kwa upande wa baadhi ya watu wa sekta ya afya wanaojipa hadhi ya kiwango fulani cha taaluma bila ya kujisajili kwenye mabaraza ya kitaaluma, Prof. Makubi ametoa miezi mitatu kwa wale wanataaluma wenye vyeti vyao wajisajilii ili kutambulika wapo katika kiwango fulani cha taaluma. 

“Kuna baadhi ya wataaluma wanaojipa hadhi ya kiwango fulani cha kitaaluma wakati hawajasajili vyeti vyao  kwenye mabaraza, nitoe mfano kuna wanataaluma wanaojiita mabingwa wa kitu fulani (specialist, consultant …) na wanajitangaza kwa wananchi wakati hatuna ushahidi na kumbukumbu. Kwahiyo tumekubaliana na mabaraza suala hilo sasa lifikie mwisho na wote waliojiendeleza zaidi waje wajisajili haraka kwa kuwasilisha vyeti vyao.” Alisisitiza Prof. Makubi.

Hata hivyo Mganga Mkuu wa Serikali aliwaagiza waganga wakuu wa mikoa, wilaya, wakurugenzi wa Hsopitali, taasisi za afya, vyuo vya afya na waganga wafawidhi wote kuzingatia kusimamia utekelezaji wa maagizo haya kwenye sekta zote za afya ili kulinda viwango na hadhi ya taaluma husika. “Taaluma zote za afya lazima ziendelee kuheshimika na kusimamiwa vizuri ili kulinda afya za wananchi kwa viwango vya juu na bila kuruhusu wanataaluma bubu”, Alisema Prof Makubi.

Pia kwa Waganga wa tiba asili wametakiwa kufuata utaratibu wa kujisajili pamoja na wasaidizi wao na kufuata miongozo ya utoaji wa tiba asili na tiba mbadala kwani serikali ipo tayari kuwapa ushirikiano kwa kuwasaidia malengo yao ya utoaji wa tiba asili yanafanikiwa.

-MWISHO-



Mkurugenzi wa Huduma za Kinga Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto 
Dkt. Leonard Subi

Na Gerard Chami - WAMJW, Arusha. 

Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imefanikiwa kutokomeza mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu (Cholera) hapa nchini.


Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Huduma za Kinga Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Leonard Subi wakati akizindua kikao kazi cha kufanya tathmini, maboresho na kuandaa mpango kazi wa miaka mitano katika kukabiliana na ugonjwa huo hapa nchini. 


“Tangu mwezi Julai mwaka 2019 hatuna kesi yoyote iliyotolewa taarifa ya kuwepo kwa mgonjwa wa Cholera hapa nchini. Kwa miaka kadhaa tumekua na takribani asilimia 11 ya vifo vitokanavyo na ugonjwa huu, lakini kutokana na kazi nzuri iliyofanyika katika maeneo tofauti ikiwemo kuimarishwa kwa miundombinu ya kutolea huduma za afya, upatikanaji wa dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi, kaya karibu zote nchini kuwa na vyoo safi na bora, kuimarishwa kwa usafi wa mazingira na upatikanaji wa maji safi na salama nchini kipindupindu kilipungua mpaka asilimia 1.7 na kwa kipindi cha mwaka jana hadi sasa hatuna mgonjwa aliyetolewa taarifa kabisa kuwa na maambukizi hayo.” Amesema Dkt.Subi 


Amesema, kazi iliyopo hivi sasa na inayopewa kipaumbele na Serikali kupitia Wizara ya Afya ni kuchambua kwa umakini mkubwa mpango kazi wa miaka mitano wa udhibiti wa ugonjwa huu, kufanya ufuatiliaji, tathmini na uperembaji wa afua mbalimbali za afya hapa nchini na kuja na mpango kazi wa utekelezaji kimkakati katika kudumisha hali hii hapa nchini kwani hivi sasa nchi imeingia katika uchumi wa kati hivyo ni vema kudumisha hali ya afya ya wananchi ambao ndiyo nguvu kazi ya Taifa katika kuleta maendeleo, kukuza kipato na kuboresha hali ya maisha ya mwananchi mmoja mmoja. 


Aidha Dkt.Subi amesisitiza kuendeleza utamaduni wa kunawa mikono muda wote kwa maji safi yanayotiririka na sabuni kwani unasaidia kukabiliana na maradhi mengine zaidi ya Corona ikiwa ni pamoja na kudumishwa kwa utoaji elimu ya afya kwa umma ili twende pamoja kama taifa linaloendelea kwa kasi. 


Akiongezea Dkt.Subi amesema ni vema kwa pamoja tukaendelea kuongeza nguvu na ushirikiano katika kulinda vyanzo na mikondo ya maji safi na salama kwani maji ni uhai na uhai ni afya hivyo itatusaidia kama Taifa kupambana na maradhi mbalimbali mijini na vijijini. 


Vilevile Dkt.Subi amesema suala la chanjo ya kuzuia kipindupindu kwasasa sio kipaumbele na badala yake nguvu kubwa inazidi kuwekwa katika kuimarisha miundombinu stahiki ya huduma za afya, usafi zaidi wa mazingira na upatikanaji zaidi wa maji safi kwa wananchi katika maeneo yote. 


Nae Mwenyekiti wa Kikao kazi hicho ambaye pia ni Mkurugenzi Msaidizi wa eneo la Ufuatiliaji na Udhibiti wa Magonjwa Dkt.Janeth Mghamba akitoa neno la shukrani kwa mgeni rasmi ameahidi kwa niaba ya timu za wataalamu wa afya kuendelea kuwashirikisha viongozi wa Serikali za Mitaa katika jamii wanazotoka (kata, mitaa na vijiji), kusukuma uimarishaji wa maabara katika ngazi zote; mkoa, wilaya, zahanati na halmashauri ikiwa ni pamoja na kuendelea kuwajengea uwezo wataalamu. 


Pamoja nae, Dkt.Faraja Msemwa kwa niaba ya Shirika la Afya Duniani (WHO) hapa nchini ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa umoja na mshikamano uliopo kwa kuwaweka wadau wa maendeleo karibu katika kukabiliana na majanga ya maradhi mbalimbali hapa nchini na yale yanayoikumba dunia kwa ujumla wake kwani afya ni msingi wa maendeleo ya Taifa lolote. 


Mwisho Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ndg.Gerard Chami, amewataka wanahabari kuendelea kutumia vyombo vyao ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Serikali kupitia Wizara ya Afya kuelimisha umma juu ya utunzaji wa mazingira, matumizi sahihi na utunzaji wa vyoo bora, uhifadhi wa vyanzo vya maji na kudumisha utamaduni wa kunawa mikono kwa maji safi na salama yanayotiririka na sabuni. 

Mwisho




KATIBU MKUU Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto - Idara Kuu ya Afya Prof. Mabula Mchembe akisema jambo  kwa wadau (hawapo pichani) wakati wa ufunguzi wa Siku ya Tiba ya Asili kwa Mwafrika

Dkt. Grace Magembe Mkurugenzi wa Huduma za Tiba kutoka Wizara ya Afya

Mzee Issa Mdoe Mwakilishi wa Wagaga wa Tiba asili kutoka Mkoa wa Dodoma






Na WAMJW- DOM 

KATIBU MKUU Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto - Idara Kuu ya Afya Prof. Mabula Mchembe amewaagiza Baraza la Tiba Asili na Tiba mbadala na Mamlaka zote katika Mikoa na Halmashauri nchini kusimamia usajili wa dawa za asili kwa kutoa elimu ya kutosha kwa waganga na watengeneza dawa wa tiba asili. 

Prof. Mchembe ameyasema hayo leo wakati akifungua maadhimisho ya siku ya tiba asili ya Mwafrika yaliyofanyika katika viwanja vya Mwl. Nyerere Jijini Dodoma, yenye kauli mbiu ya "Miongo miwili ya Tiba Asili Afrika 2001 mpaka 2020 Nchi zina mafanikio gani".

"Kwa maana hiyo basi nawaagiza Baraza la Tiba Asili na tiba mbadala na Mamlaka zote katika Mikoa na Halmashauri nchini kusimamia usajili wa dawa za asili kwa kutoa elimu ya kutosha kwa waganga na watengeneza dawa wa tiba asili" alisema Prof. Mabula Mchembe. 

Aliendelea kusisitiza kuwa, ni vyema Baraza la tiba asili na Mamlaka zote nchini, kushirikiana na taasisi zote zinazohusiana na tiba asili hususan Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kutokana na kuwepo kwa kitengo kinachohusiana na mimea. 

Prof. Mchembe amesema kuwa, katika kuadhimisha miaka 18 ya siku ya tiba asili ya Mwafrika, Serikali kupitia Wizara ya Afya imefanya mambo mengi ikiwemo, kuitambua huduma ya tiba asili katika Sera ya Afya kuanzia, kutungwa kwa Sheria ya tiba asili na tiba mbadala Namba 23 ya mwaka, kutengenezwa kwa kanuni na miongozo mbalimbali ya Tiba Asili na Tiba Mbadala mwaka, kuanza kutoa mafunzo kwa Waratibu na watoa huduma wa tiba asili nchini.

Aidha Prof. Mchembe, ameliagiza Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala na Mamlaka zote katika Mikoa na Halmashauri nchini kusimamia usajili wa dawa za asili kwa kutoa elimu ya kutosha kwa waganga na watengeneza dawa wa tiba asili.

Mbali na hayo Prof. Mchembe ametoa wito kwa Wataalamu wa tiba asili na tiba mbadala nchini kutumia fursa kwa kuanzisha viwanda vidogo na vya kati vya kuchakata dawa za asili kwa lengo la kuongeza ubora na hivyo thamani yake. 

"Nitoe wito kwa Waganga na wadau wa Tiba Asili kutumia fursa iliyopo ya Tanzania ya Viwanda kwa kuanzisha viwanda vidogo na vya kati vya kuchakata dawa za asili kwa lengo la kuongeza ubora na hivyo thamani yake" alisema Prof. Mchembe 

Kwa upande wake Mkurugenzi wa tiba Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Grace Magembe amesema kuwa, kupitia maadhimisho ya tiba asili kama nchi tumepata mafanikio mengi sana ikiwemo kuongezeka idadi kubwa ya wananchi wanaotumia dawa za asili hususan katika kipindi cha mlipuko wa virusi vya Corona. 

"Kupitia maadhimisho ya tiba asili, tangu tumeanza kama nchi, Luna mafanikio mengi sana yameweza kupatikana, lakini kubwa naloweza kulisemea, ni kuongezeka kwa idadi ya wananchi wanaotumia dawa zetu za asili pamoja na tiba mbadala, na mfano mzuri ni katika kipindi cha mlipuko wa ugonjwa wa Corona, kama nchi tunaweza kusimama kifua mbele na kusema tiba zetu za asili zimetutoa kwa kiwango kikubwa, " alisema. 

Aliendelea kusema kuwa, pamoja na kuendelea na utafiti wa dawa mbali mbali za asili ambazo zilitumika katika kipindi cha mlipuko wa ugonjwa wa Corona, takribani zaidi ya watu 100,018 walitumia dawa za asili, ikiwemo njia ya kujifukiza (nyungu), na kuonesha mafanikio kwa kiasi kikubwa. 

Nae Kaimu Msajili Baraza la tiba asili na tiba mbadala Wizara ya Afya Ndg. Patrick Seme amesema kuwa, hadi sasa Baraza la tiba asili na tiba mbadala limeshasajili dawa 30, huku akiweka wazi kuwa kiasi hiki cha dawa zilizosajiliwa ni kidogo ukilinganisha na uhalisia, huku akiweka wazi kuwa Baraza linaendelea kuhakikisha linasajili dawa nyingi zaidi kwa kufuata kanuni na taratibu. 

"Kama mnavyofahamu kuwa mwaka 2017 tulianza kusajili dawa za asili kupitia Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala na kuwa hadi sasa dawa 30 zimesajiliwa. Kiasi hiki cha dawa zilizosajiliwa nichache sana ukilinganisha na uhalisia." Alisema. 

Akiwawawakilisha Waganga wa tiba asili Mkoa wa Dodoma Mzee Issa Mdoe amesema kuwa, Baraza la tiba asili na tiba mbadala kwa kushirikiana na Waganga wa tiba asili limekuwa na mafanikio mengi yakiwemo kutoa elimu mara kwa mara kwa Waganga kujua dhana ya tiba asili ikiwemo kujiepusha na mauaji ya vikongwe na mauaji ya albono na mauaji ya watoto wadogo. 

Mbali na hayo Mzee Issa Mdoe ameweka wazi kuwa, baadhi ya changamoto zinazowakumba, zikiwemo gharama za usajili wa dawa kuwa juu, hivyo kuwafanya Waganga wengi kushindwa kisajili dawa zao, elimu ndogo ya malipo ya njia ya elektroniki inayopelekea baadhi ya Waganga katapeliwa na watu wasio waaminifu.

Mwisho.



Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Abel Makubi (watatu kutoka kushoto) akikagua taarifa za mgonjwa katika Hospitali ya Rufaa ya kanda ya Kaskazini KCMC, pindi alipofanya ziara ya kukagua hali ya utoaji huduma katika Hospitali hiyo.

Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Abel Makubi (watatu kutoka kushoto) akipokea taarifa za hali ya mgonjwa katika Hospitali ya Rufaa ya kanda ya Kaskazini KCMC, pindi alipofanya ziara ya kukagua hali ya utoaji huduma katika Hospitali hiyo.
Kiwanda cha uzalishaji mitungi ya oksijeni kilichopo katika Hospitali ya Rufaa ya kanda ya kaskazini KCMC. 

Baadhi ya mashine za uzalishaji wa gesi ya oksijeni inazotumika katika matibabu  ya wagonjwa katika Hospitali ya Rufaa ya kanda ya kaskazini KCMC.


TUSHIRIKIANE KUPAMBANA DHIDI YA MAGONJWA YASIYO AMBUKIZA - MGANGA MKUU WA SERIKALI.

Na WAMJW- KILIMANJARO

MGANGA Mkuu wa Serikali Prof. Abel Makubi ametoa wito kwa watoa huduma za Afya kushirikiana kwa pamoja kwa kutoa elimu, katika mapambano dhidi ya magonjwa yasiyo ambukiza yanayosababishwa na mtindo wa maisha ikiwemo ulaji usiofaa, matumizi ya vileo na kutofanya mazoezi.

Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Makubi ametoa rai hiyo wakati alipotembelea Hospitali ya Rufaa ya kanda ya Kaskazini KCMC kukagua hali ya utoaji huduma za Afya katika Hospitali hiyo kwa wananchi.

Prof. Makubi amesema kuwa, ni muhimu watoa huduma za afya kuungana kwa pamoja kushirikiana kwa kutoa elimu kwa wananchi kuhusu magonjwa yasiyo ambukiza (NCD), kupitia njia yakuwafuata wagonjwa katika maeneo yao, jambo ambalo litasaidia kupunguza mzigo wa wagonjwa katika hospitali za Rufaa nchini.

"Mshirikiane kwa pamoja kutoa Elimu ya ufahamu, na kupima angalau mara 2 kwa mwaka juu ya  magonjwa yasiyo ambukiza (NCD) kupitia njia ya kuwafuata wateja katika maeneo yao na kuwafanyia upimaji (outreach program)" alisema Prof. Makubi.

Hata hivyo, Prof. Makubi ametoa rai kwa watoa huduma za afya kuhakikisha wanatoa huduma kwa wakati kwa wagonjwa ili kuepusha msongamano unaoweza sababisha mlipuko wa magonjwa mengine katika hospitali na kupunguza usumbufu kwa wagonjwa.

Aidha, Prof. Makubi ameridhishwa kwa kiasi kikubwa hali ya utoaji huduma katika Hospitali hiyo, huku akiwataka kuongeza jitihada ili kutoa huduma bora zaidi kwa wananchi na kupunguza malalamiko yanayoweza kuepukika kwa urahisi.

"Mimi kwa KCMC, sipati malalamiko mengi sana, simamìeni katika ubora huo, na mhakikishe mnaongeza Juhudi zaidi, na kwa hilo nawapongèza sana sana" alisema Prof. Abel Makubi.

Hata hivyo, Prof. Makubi amewapongeza watumishi wa Hospitali ya KCMC wakiongozwa na Mkurugenzi wao Prof. Gileard Masenga kwa kuanzisha mradi wa uzalishaji wa gesi ya oksijeni, jambo linalosaidia kuongeza mapato na kuokoa kiasi kikubwa cha pesa ambacho kingetumika kununua mitungi ya gesi, na pesa hizo kuelekezwa katika kuboresha huduma kwa wananchi.

Nae, Mkurugenzi wa huduma za tiba Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Grace Maghembe amewataka kutobweteka, katika kuwahudumia wananchi, licha ya kazi nzuri ambayo inaendelea kufanywa na uongozi kwa kushirikiana na Mkoa.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa uhakika ubora huduma Wizara ya Afya Dkt. Eliakim Eliud amewataka watoa huduma kuhakikisha wanafuata miongozo ya kujikinga ya utoaji huduma (IPC guidelines) wakati wa kuhudumia wagonjwa ili kujikinga wao na wagonjwa wanaowahudumia.

Mwisho.



Mkurugenzi wa Tiba Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na watoto Dkt. Leonard Subi, akisisitiza jambo mbele ya Waandishi wa habari wakati alipofanya ziara katika ghara la chanjo lililopo katika Hospitali ta Rufaa ya Mkoa wa Dodoma-General.


HATUNA UHABA WA CHANJO NCHINI: DKT. LEONARD SUBI

Na. Catherine Sungura,WAMJW-Dodoma

Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imesema kuwa, haina upungufu wa chanjo wa aina yeyote hivyo kuwataka wazazi/walezi kuwapeleka watoto wao kuwapatia chanjo katika vituo vya kutolea huduma za afya.

Hayo yamesemwa leo na Mkurugenzi wa Kinga kutoka Wizara ya Afya Dkt. Leonard Subi wakati alipotembelea ghala ya kuhifadhia chanjo iliyopo hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma kukagua hali ya chanjo katika mkoa huo.

Dkt. Subi amesema kuwa, chanjo zote aina tisa ambazo zinakinga dhidi ya magonjwa kumi na tatu zipo kwenye ghala hilo“tulikua na upungufu wa aina mbili za chanjo nchini kati ya tisa ambazo tumekuwa tukizitoa lakini, sasa hivi chanjo zote zipo, kwani zimeshawasili hapa nchini na usambazaji unaendelea”, amesema Dtk. Subi

Hata hivyo Dkt. Subi amesema kuwa, upungufu huo wa chanjo ulitokea baada ya Dunia kukumbwa na janga la mlipuko wa ugonjwa wa COVID-19 ambapo anga zote zilifungwa kwani chanjo husafirishwa kwa mnyororo baridi, kwahiyo huitaji usafiri wa anga.

“Tunamshukuru Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwa kulifungua anga la Tanzania ambapo,  chanjo sasa zimeanza kuingia nchini na hadi sasa mikoa kumi na tatu(13) chanjo hizi zimeshapokelewa kati ya mikoa 26, na mikoa mingine kumi na tatu  ya Tanzania Bara usambazaji unaendelea kupitia Bohari ya Dawa (MSD)”.

Aidha, Dkt. Subi alisema kuwa, usambazaji wa chanjo hizo mbili ambazo wananchi walikua wanazikosa, umeshaanza na watazipata kwa uhakika, huku akielekeza bohari ya dawa nchini (MSD) kuhakikisha chanjo zote  zimefika katika mikoa iliyosalia ya Tanzania Bara ifikapo mwishoni mwa wiki hii.

“Waganga Wakuu wa Mikoa na Halmashauri wote nchini hakikisheni chanjo hizo mnazipeleka kwenye vituo vyetu  vya kutolea huduma za afya na muwajulishe wananchi kwamba chanjo zipo na zinapatikana bila malipo yeyote, wazazi na walezi pelekeni watoto wenu kupata chanjo katika mikoa yenu”Alisisitiza Dkt. Subi.

Kwa upande wa taarifa iliyotolewa na moja ya chombo cha habari hapa nchini kwa kukosekana kwa chanjo ya kuzuia kuhara (Rota) Dkt. Subi alifafanua kuwa, nchi ya Tanzania haijawahi kukosa chanjo hiyo,huku akiweka bayana kuwa, chanjo zilizopungua kwa mwezi mmoja na nusu ni chanjo ya Polio na Surua-Rubella hali iliyosababishwa na mlipuko wa Covid-19 Duniani, huku akisisitiza kuwa serikali imekua ikinunua chanjo hizo kutoka nchi za Ulaya na Asia.

Aliendelea kusema kuwa, Serikali inaendelea kutoa fedha za chanjo, na kuweka wazi kuwa hadi sasa  imetoa zaidi ya  shilingi bilioni 18 kwa ajili ya ununuzi wa chanjo  na kuifanya  Tanzania kuendelea kuwa katika kiwango cha juu cha utoaji wa chanjo kwa zaidi ya asilimia 98 kwa miaka sita mfululizo.

Hata hivyo, Dkt. Subi amesema kuwa, Tanzania haijawahi kupata mgonjwa wa kupooza tangu mwaka 1996, jambo linalotokana na  uwepo wa hali nzuri ya upatikanaji wa chanjo, huku akidai kuwa nchi ya Tanzania tayari imepata cheti cha utambuzi kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO) mwaka 2015.

 

MWISHO.



MKRdezign

{facebook#YOUR_SOCIAL_PROFILE_URL} {twitter#YOUR_SOCIAL_PROFILE_URL} {google-plus#YOUR_SOCIAL_PROFILE_URL} {youtube#YOUR_SOCIAL_PROFILE_URL} {instagram#YOUR_SOCIAL_PROFILE_URL}

Contact Form

Name

Email *

Message *

Powered by Blogger.
Javascript DisablePlease Enable Javascript To See All Widget