Prof. Abek Makubi Katibu Mkuu Wizara ya Afya
Na. WAMJW - Dodoma.
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imeanza kutekeleza kwa kasi maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ikiwa ni sehemu ya maboresho ya utoaji huduma katika Sekta ya Afya.
Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu Wizara ya Afya - Idara Kuu Afya Prof. Abel Makubi katika kikao na Watumishi wa Idara Kuu ya Afya Makao Makuu kilichofanyika katika ukumbi wa Hazina Jijini Dodoma.
Katika kutekeleza maagizo hayo Prof. Makubi amesema kuwa, Wizara inategemea kuwasilisha Bungeni mchakato wa kuridhiwa kwa Bima ya Afya kwa wote ili uweze kupitishwa na kuwezesha wananchi wote kuwa na Bima ya Afya hali itakayosaidia kupunguza gharama za matibabu kwa wananchi wote.
"80% ya Watanzania ni watoto wa wakulima, Wizara imepeleka mchakato huu haraka bungeni ili uweze kupitishwa, ambapo utasaidia wananchi wote kuwa na Bima ya Afya, jambo litalosaidia kupunguza gharama za matibabu kwa wananchi," amesema Prof. Makubi.
Aliendelea kusema kuwa, Serikali inaendelea kuweka mikakati mizuri itayosaidia wananchi ambao hawatakuwa na uwezo wa kulipa kiasi hicho ili kupata Bima ya Afya kwa kutafuta vyanzo vingine vya fedha ili kuwalipia huduma hiyo.
Hata hivyo, Prof. Makubi amesema kuwa, katika miaka mitano iliyopita Serikali imejenga vituo vya kutolea huduma za Afya vya kutosha ikiwemo Hospitali za Kanda, Hospitali za Wilaya, Hospitali za Rufaa za Mikoa, Vituo vya Afya na Zahanati, na hivyo katika kutekeleza agizo hilo amesema Wizara inaendelea kuhakikisha maboma yote yanakamilika na kuanza kutoa huduma za Afya kwa wananchi kwa kiasi kidogo cha fedha ndani ya miundombinu yenye ubora.
Kwa upande mwingine amesema kuwa, licha ya malalamiko kutoka kwa wananchi juu ya hali ya upatikanaji wa dawa kutoridhisha nchini, Wizara ya imepokea jumla ya Tzs.Bilioni 80 kutoka Serikalini ili kuboresha hali ya upatikanaji wa dawa kwa wananchi. Ameonya kuwa Serikalini haitakubali kuona fedha hizi zinatumiwa vibaya au dawa kuibiwa katika vituo vya kutolea huduma.
Aliendelea kusema kuwa, katika kuimarisha zaidi eneo hilo, Wizara imekutana na Wazabuni ili kuendelea kuimarisha hali ya upatikanaji wa dawa, jambo litalosaidia kupunguza changamoto za malalamiko yanayotokana na ufinyu wa huduma za dawa katika vituo vya kutolea huduma.
Kuhusu masilahi ya watumishi, Profesa Makubi alisisitiza maelekezo ya Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan kuhakikisha “motivations” zinatolewa , hasa kwa kazi nzuri zinazofanyika. Ameelekeza Taasisi zote chini ya Sekta ya Afya kwa moyo wa shukurani na pongezi kwa watumishi wanaojituma kupitia haki zao, mapato ya ndani, na miradi mbalimbali pale ambapo miongozo inaruhusu .
Aidha, Prof. Makubi amesema kuwa, moja kati ya kipaumbele cha Wizara ya Afya ni kupunguza vifo vya mama na mtoto wakati wa kuleta kiumbe kipya Duniani, hivyo kuwataka Watumishi wa Wizara ya Afya kwa kushirikiana na OR TAMISEMI kusimamia huduma bora ili kupunguza vifo hivyo ikiwezekana kuviondoa kabisa.
"Ni wajibu wetu kupunguza vifo vya mama na mtoto, naomba hili tulisimamie wote, nisingependa kuona vifo vya mama, wakati analeta kiumbe kipya Duniani," alisema Prof. Abel Makubi.
Kwa upande mwingine, Prof. Makubi amesema kuwa, Wizara imeendelea kuhamasisha wananchi kushiriki katika mapambano dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza kwa kuboresha mtindo wa maisha ikiwemo kufanya mazoezi, kula mlo unaofaa na kupata elimu juu ya kujikinga dhidi ya magonjwa hayo.
Aliendelea kwa kutoa maelekezo ya kuongeza kasi katika kutoa elimu kwa wananchi hususan watoto ili kujenga tabia ya kupenda kufanya mazoezi na kufuata mlo kamili, huku akiwaasa Watumishi wa Afya kuwa mstari wa mbele kwa kufanya mazoezi na kutoa elimu kwa wananchi.
Aliendelea kwa kuwapongeza Watumishi wote wa Sekta ya Afya kwa namna walivyoshiriki katika mapambano dhidi ya magonjwa ya kuambukiza ikiwemo magonjwa ya mlipuko kama vile ugonjwa wa Corona, huku akiwataka kuendelea kujikinga dhidi ya ugonjwa huo kwa kuchukua tahadhari zote muhimu kama kunawa mikono kwa sabuni na maji safi yanayotiririka, kuvaa barakoa pale panapohitajika na kuepuka msongamano isiyo ya ulazima.
Hata hivyo, Prof. Makubi amesisitiza juu ya kuongeza kasi katika kuboresha huduma za tiba asili, huku akielekeza kuwa na kituo cha Kisasa cha Tiba Asili kitachorahisisha shughuli zote ikiwemo tafiti kuhusu tiba asili na kuweka wazi kuwa dawa za tiba asili ziweze kupatikana katika maduka ya dawa (famasi).
Huduma kwa wateja, ni sehemu nyingine ambayo Prof. Makubi amesisitiza iongeze kasi kwa Watumishi, huku akielekeza Huduma kwa Wateja (Customer Care) zianze kutolewa kwa wateja mara wanapoingia getini au mlango mkuu mpaka wanapomaliza kupokea huduma na kuondoka.
"Huduma nzuri kwa wateja zianze kwetu ndani ya Wizara, wageni wapokelewe vizuri kuanzia getini, hatupendi kusikia malalamiko ya watu hawajapokelewa vizuri, wote tuna nafasi ya kupokea na kuwasikiliza wateja pindi wanapokuja kuhitaji huduma," amesema.
Pia, Prof. Makubi ameagiza kuongezeka kwa kasi ya kushughulikia kero kutoka kwa wananchi ili waweze kupata huduma kwa haraka, aliendelea kusema kuwa kila mtumishi kwa nafasi yake ahakikishe anashughulikia kero za wananchi ili zisifike ngazi ya viongozi wa juu.
Mwisho.