November 2020

Mkurugenzi wa huduma za kinga Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Leonard Subi akisisitiza jambo mbele ya Waganga Wakuu wa Mkoa na Waratibu wa Kifua Kikuu na Ukoma wakati wa kuhitimisha Mkutano wa mwaka wa Kifua Kikuu na Ukoma uliofanyika Jijini Dodoma.

Mkurugenzi msaidizi wa Idara ya Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe TAMISEMI Dkt. Paul Chawote akieleza jambo wakati wa kuhitimisha Mkutano wa mwaka wa Kifua Kikuu na Ukoma uliofanyika Jijini Dodoma.

Meneja Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Kifua Kikuu na Ukoma nchini Dkt. Zuweina Kondo Sushy akifuatilia neno kutoka kwa Mkurugenzi wa huduma za kinga Wizara ya Afya (hayupo kwenye picha) wakati wa kuhitimisha Mkutano wa mwaka wa Kifua Kikuu na Ukoma uliofanyika Jijini Dodoma.

Waganga Wakuu wa Mikoa na Waratibu wa Kifua Kikuu na Ukoma wakimkaribisha mgeni rasmi (hayupo kwenye picha), wakati wa kuhitimisha Mkutano wa mwaka wa Kifua Kikuu na Ukoma uliofanyika Jijini Dodoma.



Na Rayson Mwaisemba WAMJW- DOM 

Mkurugenzi wa kinga Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Leonard Subi ametoa wito kwa Waganga Wakuu wa mikoa wote kutumia mbinu mbali mbali ili kuutokomeza ugonjwa wa ukoma na Kifua Kikuu nchini Tanzania. 

Dkt. Subi ametoa wito huo leo wakati akifunga Mkutano wa mwaka wa Mpango wa taifa wa kudhibiti kifua Kikuu na ukoma uliohudhuriwa na Waganga wakuu na Waratibu wa kifua Kikuu na ukoma ngazi ya Mkoa, uliofanyika Jijini Dodoma. 

"Tumieni kila liwezekanalo ugonjwa wa ukoma uishe nchini Tanzania, kwa Waganga Wakuu wa Mkoa ambao Halmashauri zenu bado zina maambukizi ya ukoma jipeni ndani ya miaka mitano ugonjwa wa ukoma utoweke nchini " amesema Dkt. Subi. 

Dkt. Subi amesema kuwa, ni muhimu kwa viongozi kutumia takwimu ili kuwasaidia katika kufanya maamuzi sahihi na kwa wakati katika utekelezaji wa majukumu yao, jambo litalosaidia kutokomeza maambukizi ya ugonjwa wa Kifua Kikuu na Ukoma nchini. 

Aidha, Dkt. Subi ametoa agizo kwa Waganga Wakuu wa mikoa wote kuhakikisha maelekezo na maazimio yaliyotokana na Mkutano huo yatolewe kwa maandishi kwa Halmashauri zote nchini ikiwa ni sehemu ya mikakati ya kutokomeza ugonjwa wa Ukoma na Kifua Kikuu.

Mbali na hayo, Dkt. Subi ameagiza kuendelea kutoa elimu ya Afya kwa umma kwa wananchi kupitia vyombo vya habari kama vile radio za jamii, mitandao ya jamii, ili kuwakinga wananchi wetu dhidi ya maambukizi ya magonjwa ikiwemo ugonjwa wa Kifua Kikuu na Ukoma. 

"Toeni elimu ya Afya kwa wananchi, wananchi waelimishwe kuhusu magonjwa mbali mbali katika Jamii ikiwemo ugonjwa wa Kifua Kikuu na Ukoma, wekeni utaratibu wa vipindi vya Afya kwenye radio za mikoa yenu" amesema Dkt. Subi. 

Kwa upande wake Mkurugenzi msaidizi wa Idara ya Afya na Ustawi wa Jamii na Lishe TAMISEMI Dkt. Paul Chawote amemhakikishia Mgeni rasmi kusimamia utekelezaji wa maazimio ya Mkutano huo ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kutokomeza maambukizi ya ugonjwa wa Kifua Kikuu na ukoma nchini. 

"Sisi kama Ofisi ya Rais TAMISEMI tumejipanga kusimamia utekelezaji wa maazimio yote ambayo yametokana na Mkutano huo ili kupambana dhidi ya ugonjwa wa Kifua Kikuu na Ukoma nchini "amesema Dkt. Çhawote. 

Mwisho



Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Prof. Mabula Mchembe akifungua Mkutano wa saba wa Afya uliohudhuriwa na Wadau mbali mbali wa Sekta ya Afya nchini, Jijini Dodoma.

Mkurugenzi Idara ya Afya ustawi wa Jamii na Lishe Dkt. Ntuli Kapologwe akimkaribisha mgeni rasmi, Katibu Mkuu Wizara ya Afya Prof. Mabula Mchembe (hayupo kwenye picha) wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa saba wa afya, uliohudhuriwa na Wadau mbali mbali wa afya nchini, Jijini Dodoma

Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Prof. Mabula Mchembe akipita katika banda la NIMR kujionea shughuli zinazoendelea, wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa saba wa Afya uliohudhuriwa na Wadau mbali mbali wa Sekta ya Afya nchini, Jijini Dodoma.

Wadau mbali mbali wa masuala ya Afya waliohudhuria Mkutano wa saba wa masuala ya Afya unaoendelea Jijini Dodoma kujadili namna bora ya kuboresha huduma za Afya nchini.

Picha ya pamoja ikiongozwa na Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Prof. Mabula Mchembe akiwa na Wadau mbali mbali wa Afya wakati wa  Mkutano wa saba wa Afya unaoendelea Jijini Dodoma.



PROF. MCHEMBE AWAAGIZA WATAALAMU WA SEKTA YA AFYA KUFIKIRIA HUDUMA BORA NA NAFUU KWA WANANCHI

Na Rayson Mwaisemba, WAMJW - DOM 

KATIBU Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Prof. Mabula Mchembe ametoa wito kwa Wataalamu wa Sekta ya Afya nchini kuhakikisha wanafikiria namna ya utoaji huduma bora na kwa gharama nafuu ili wananchi wenye hali zote waweze kuzimudu.

Wito huo ameutoa leo, wakati akifungua Mkutano wa saba wa Sekta ya Afya uliohudhuriwa na Watumishi kutoka Wizara ya Afya, Ofisi ya Rais TAMISEMI na Wadau mbali mbali wanaojihusisha na masuala ya Afya nchini.

"Ni wajibu wetu sisi, tukiwa kwenye Mkutano huu wa wa Afya kuwaza vyema tunamsaidiaje mwananchi wa hali ya chini kupata huduma bora, zenye unafuu na zinazofikika kila sehemu bila kumuumiza mwananchi" alisema Prof. Mchembe.

Hata hivyo, Prof. Mchembe amesema kuwa, Wizara ya Afya itaendelea kutoa ushirikiano kwa Wadau wote ili kufanikisha utoaji huduma bora na nafuu kwa wananchi, huku akiweka wazi kuwa kama Serikali itatendea kazi mapendekezo na ushauri utakaotokana na Mkutano huo. 

Aidha, Prof. Mchembe amesisitiza kuwa, ni muhimu mijadala itayoendelea katika Mkutano huo kuhakikisha inapita kwenye malengo ya Wizara yakiwemo kupunguza vifo vya mama na mtoto, kupunguza maambukizi ya VVU, TB, Ukoma, 

Mbali na hayo, Prof. Mabula Mchembe amewataka Wataalamu hao kujadili masuala ya kupunguza magonjwa yasiyo yakuambukiza ambayo yanaongeza mzigo kwa Serikali kutokana na gharama za kuyatibu magonjwa hayo, yanayotokana na mtindo wa maisha ikiwemo matumizi ya pombe kupita kiasi, kutofanya mazoezi. 

Naye, Mkurugenzi Idara ya Afya ustawi wa Jamii na Lishe kutoka TAMISEMI Dkt. Ntuli Kapologwe amesema kuwa, Serikali imefanya maboresho mengi sana katika miaka saba iliyopita, huku akiweka wazi kuwa mambo yatakayojadiliwa katika kikao hicho yataendana na mpango mkakati wa Sekta afya unaosimamiwa na Serikali kupitia Wizara ya Afya. 

Pia, Dkt.Kapologwe amesema kuwa, kama wasimamizi wa Sera watahakikisha maazimio yatakayotoka kwenye kikao hicho yanaingizwa kwenye mipango ya utekelezaji kwenye Hospitali zote ngazi ya Wilaya, Halmashauri na zahanati kwa utekelezaji zaidi. 

"Katika kikao hiki, pamoja na maelekezo ambayo utayatoa, sisi tukiwa kama wasaidizi wako tutahakikisha, maelekezo yako pamoja na maazimio utakayotoa katika kikao hiki, tunaenda kuyaingiza katika mipango yetu katika Hospitali za Mikoa, Halmashauri na Zahanati" amesema Dkt. Ntuli Kapologwe. 

Mwisho



Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Prof. Mabula Mchembe akifungua Mkutano wa 21 wa Kitaalam wa Tathmini ya Utekelezaji katika Sekta ya Afya uliohudhuriwa na Wadau wa Sekta ya Afya nchini, Jijini Dodoma.

Naibu Katibu Mkuu TAMISEMI anaeshughulikia masuala ya Afya Dkt. Dorothy Gwajima akieleza jambo wakati wa ufunguzi  wa Mkutano wa 21 wa Kitaalam wa Tathmini ya Utekelezaji katika Sekta ya Afya uliohudhuriwa na Wadau wa Sekta ya Afya nchini, Jijini Dodoma.

Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Abel Makubi akimkaribisha mgeni  rasmi Katibu Mkuu Wizara  ya Afya Prof. Mabula Mchembe (hayupo kwenye picha) wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa 21 wa Kitaalam wa tathmini ya utekelezaji katika Sekta ya Afya uliohudhuriwa na Wadau wa Sekta ya Afya nchini, Jijini Dodoma.

Wakurugenzi kutoka Wizara ya Afya wakiteta jambo wakati  wa ufunguzi wa Mkutano wa 21 wa Kitaalam wa tathmini ya utekelezaji katika Sekta ya Afya uliohudhuriwa na Wadau wa Sekta ya Afya nchini, Jijini Dodoma.

Baadhi ya Wakurugenzi wasaidizi kutoka Wizara ya Afya  walioshiriki katika ufunguzi wa Mkutano wa 21 wa kitaalam wa tathmini ya utekelezaji katika Sekta ya Afya uliofanyika Jijini Dodoma.

Baadhi ya Wadau waliohudhuria ufunguzi wa Mkutano wa 21 wa Kitaalam wa tathmini ya utekelezaji katika Sekta ya Afya uliofanyika Jijini Dodoma.

Wakurugenzi kutoka Wizara ya Afya na Wadau wa Sekta ya Afya nchini walio hudhuria  ufunguzi wa Mkutano wa 21 wa Kitaalam wa tathmini ya utekelezaji katika Sekta ya Afya uliofanyika Jijini Dodoma.

Picha ya pamoja ikiongozwa na Katibu Mkuu Wizara  ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Prof. Mabula Mchembe, akiwa na Sekretarieti ya mkutano wa 21 wa Kitaalam wa tathmini ya utekelezaji katika Sekta ya Afya.



Na, Rayson Mwaisemba WAMJW- DOM 

SERIKALI, kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imeendelea kujidhatiti katika kuboresha utoaji huduma za Afya kwa wananchi ikiwemo kupunguza vifo vya mama na mtoto, uboreshaji wa huduma za chanjo, upatikanaji wa vifaa na vifaa tiba. 

Hayo yamesemwa leo na Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Prof. Mabula Mchembe wakati akifungua Mkutano wa 21 wa kitaalam wa tathmini ya utekelezaji katika Sekta ya Afya ulioandaliwa kwa pamoja na Wizara yake na Ofisi ya Rais TAMISEMI ukishirikisha Wadau mbalimbali wa Sekta ya Afya nchini unaoendelea Jijini Dodoma.

Prof. Mchembe amesema kuwa, kikao hicho kina umuhimu mkubwa sana katika Wizara na Sekta ya Afya kwa ujumla kwa sababu ndio kinachoweza kuweka mikakati ya nini kifanyike miaka mitano ijayo, baada ya kupitia mikakati ya miaka mitano iliyopita na kuona mafanikio na changamoto zake.

"Kama Serikali tumefanikiwa kuboresha katika kupunguza vifo vya mama na mtoto,  huduma za chanjo, vifaa na vifaa tiba pamoja na uboreshaji wa utoaji huduma zinazotolewa na Watumishi wa Afya" amesema Prof. Mchembe. 

Aidha,  Prof. Mchembe amesema mpango mkakati wa tano unaoenda kuanza ni matokeo ya ule wa nne ambapo unaangazia mafanikio, na kuboresha maeneo yaliyokuwa na changamoto na kuweka mikakati madhubuti ya kuboresha Sekta ya Afya. 

Naye Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia masuala ya Afya kutoka ofisi ya Rais TAMISEMI Dkt. Dorothy Gwajima amesema kuwa, kama wasimamiaji wa utekelezaji wa Sera katika ngazi za Mikoa na Mamlaka za mitaa wapo tayari kutekeleza maagizo na miongozo itayotolewa kupitia kikao hicho cha tathmini ya Sera kilichohudhuriwa na Wadau wote wa Sekta ya Afya nchini. 

"Katibu Mkuu Wizara ya Afya ameeleza mambo mengi, sisi tupo kama Wadau ambao tunasimamia utekelezaji kwenye ngazi ya Mikoa na Mamlaka ya Serikali za Mitaa tunasubiri maelekezo  na miongozo ya Kisera ili kwenye kipindi cha miaka mitano ijayo tuweze kutekeleza kwa kasi ile ile" alisema Dkt. Gwajima. 

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Sera na Mipango Wizara ya Afya Bw. Edward Mbanga amesema kuwa, kikao hicho cha Sera hupokea mambo yote katika Sekta ya Afya yaliyofanyiwa tathmini na yaliyokubalika kuwa ndio yatakuwa malengo na muelekeo wa Sekta ya Afya nchini. 

Mwisho.


MKRdezign

{facebook#YOUR_SOCIAL_PROFILE_URL} {twitter#YOUR_SOCIAL_PROFILE_URL} {google-plus#YOUR_SOCIAL_PROFILE_URL} {youtube#YOUR_SOCIAL_PROFILE_URL} {instagram#YOUR_SOCIAL_PROFILE_URL}

Contact Form

Name

Email *

Message *

Powered by Blogger.
Javascript DisablePlease Enable Javascript To See All Widget